Yemen; maabara ya silaha zilizopigwa marufuku za Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64651-yemen_maabara_ya_silaha_zilizopigwa_marufuku_za_magharibi
Abdul-Qadir Antar, mshauri wa Waziri Mkuu wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, nchi hiyo imegeuzwa kuwa maabara na mahapa pa kujaribia silaha zilizopigwa marufuku za Magharibi.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Nov 16, 2020 03:32 UTC
  • Yemen; maabara ya silaha zilizopigwa marufuku za Magharibi

Abdul-Qadir Antar, mshauri wa Waziri Mkuu wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, nchi hiyo imegeuzwa kuwa maabara na mahapa pa kujaribia silaha zilizopigwa marufuku za Magharibi.

Imepita miezi 68 sasa tangu muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uanzishe vita vyake dhidi ya Yemen. Vita hivi vimekuwa na matokeo mbalimbali. Hata hivyo utumiaji wa silaha zilizopigwa marufuku ni moja ya matukio mabaya na ya kusikitisha zaidi. Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha vita vyake vya miezi 68 dhidi ya Yemen, muungano huo vamizi umetumia silaha mbalimbali ambazo zimepigwa marufuku.

Mabomu ya vishada, silaha za vijidudu, fosforasi, kemikali, mabomu ya moto, mabomu yanayozalisha joto, sumu ya mvuke na aina kwa aina ya mabomu zikiwemo silaha zilizopigwa marufuku ni baadhi ya silaha zilizotumiwa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudia katika kipindi cha miezi 68 ya vita dhidi ya Yemen. Huko nyuma pia, asasi mbalimbali za haki za binadamu zimewahi kuituhumu Saudia kwamba, imekuwa ikitumia mabomu ya vishada dhidi ya raia wa Yemen.

 

Katika uwanja huo, Rupert Colville, msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umetumia mabomu ya vishada huko Yemen ambayo kimsingi yamepigwa marufuku. Kwa mujibu wa mkataba wa silaha uliopasishwa mwaka 2008 na kusainiwa na takribani nchi 100, mabomu hayo yalikatazwa na kupigwa marufuku.

Nukta muhimu katika kadhia hii ni kwamba, silaha hizi zilizopigwa marufuku zinatengenezwa Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Amani (Stockholm International Research Institute) kimetangaza kuwa, kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 Marekani imekuwa mdhamini mkubwa wa zana za kijeshi za utawala wa Aal Saud na asilimia 73 ya silaha za Saudia zinatoka Marekani.

Kuanzia mwaka 2015 hadi 2019, asilimia 25 ya mauzo yote ya silaha za Marekani nje ya nchi yalikwenda Saudia. Uingereza nayo kuanzia Januari mwaka 2015 hadi sasa imetoa kibali cha kuuziwa silaha utawala wa Riyadh zenye thamani ya pauni bilioni 6.4.

Hujuma na mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen

 

Hamid Abdu-Qadir Antar mchambuzi wa masuala ya kisisa na kistratejia na ambaye pia ni mshauri wa Waziri Mkuu wa Serikali ya wokovu wa Kitaifa ya Yemen anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Vikosi vya anga vyenye mfungamano na muungano wa kimataifa wa kijeshi vimeruka mara milioni moja katika kipindi cha miaka sita ya vita dhidi ya Yemen.

Mashirika yanayozalisha silaha nchini Marekani na Uingereza yameifanya Yemen kuwa mahala pa kufanyia majaribio ya silaha zao. Katika vita hivi, wananchi wa Yeme wamevurumishiwa na kumiminiwa silaha zilizopigwa marufu, zinazoua na zenye uharibifu mkubwa. Silaha hizo mbali na mauaji zimebomoa na kusambaratisha kabisa miundomsingi na kubomoa nyumba za Wayemen.

Matokeo ya kutumia silaha zilizopigwa marufuku dhidi ya wananchi wa Yemen ni kutokea maafa makubwa ya kibinadamu kuwahi kushuhudiwa katika miongo ya hivi karibuni. Mbali na makumi ya maelfu ya raia kuuawa na kujeruhiwa, vita hivyo vimesababisha kushadidi maradhi mbalimbali.

Jinai za Saudia huko Yemen

 

Taha al-Mutawakkil, Waziri wa Afya wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema, tangu kuanza hujuma na uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen, idadi ya wagonjwa wa saratani katika maeneo yaliyoshambuliwa kwa silaha zilizopiwa marufuku imeongezeka kwa asilimia mia moja. Aidha waziri huyo ametangaza kuwa, matatizo ya ubongo na kisaokolojia baina ya wananchi wa Yemen nayo yameongezeka ikiwa ni natija ya kushadidi mashambulio ya muungano vamizi wa Saudia.

Wakati huo huo, Muhammad al-Zubairi, Waziri wa Uvuvi wa Yemen naye ametangaza kuwa, sekta ya uvuvi nchini humo imepata hasara ya kwa akali dola bilioni 9 kutokana na kushuhudiwa hujuma na mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake. Kwa upande wake, Zakaria al-Shami, Waziri wa Usafiri na Uchukuzi wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ametangaza kwamba, sekta ya usafiri na uchukuzi ya nchi hiyo imepata hasara ya kwa uchache dola bilioni 5 na milioni 856.

Licha ya kuweko hasara za kibinadamu na zisizo za kibinadamu ambazo ziko wazi na bayana kabisa sambamba na kutumiwa mara chungu nzima silaha zilizopigwa marukufu huko nchini Yemen, lakini kimya ndio radiamali muhimu kabisa ambayo imeonyeshwa na jamii ya kimataifa mkabala wa jinai hizi za kutisha.