UN yalaani hatua ya Israel ya kuendelea kuua watoto wa Kipalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65259-un_yalaani_hatua_ya_israel_ya_kuendelea_kuua_watoto_wa_kipalestina
Wataalamu wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamelaani vikali kitendo cha wanajeshi wa utawala haramu wa Israel cha kumuua kijana mwingine wa Kipalestina, huo ukiwa ni muendelezo wa mauaji dhidi ya watoto wa Kipalestina yanayofanywa na Wazayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 18, 2020 03:50 UTC
  • UN yalaani hatua ya Israel ya kuendelea kuua watoto wa Kipalestina

Wataalamu wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamelaani vikali kitendo cha wanajeshi wa utawala haramu wa Israel cha kumuua kijana mwingine wa Kipalestina, huo ukiwa ni muendelezo wa mauaji dhidi ya watoto wa Kipalestina yanayofanywa na Wazayuni.

Katika taarifa ya pamoja ya jana Alkhamisi, Michael Lynk, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu tokea mwaka 1967, na Agnès Callamard, Ripota Maalumu wa umoja huo katika masuala ya mauaji ya kiholela imekosoa vikali mauaji hayo ya mtoto wa Kipalestina ambayo ni ya sita mwaka huu 2020.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kuuawa na wanajeshi wa Israel Ali Ayman Abu Aliya, kijana wa miaka 15 katika maandamano yaliyofanyika mapema mwezi huu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan katika hali ambayo hakuwa tishio kwa maafisa usalama wa Israel, ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Habari ya Palestina, watoto 3,097 wa Palestina wameuawa shahidi na wanajeshi wa Israel tangu ilipoanza Intifadha ya Pili inayojulikana kama Intifadha ya al-Aqsa miaka 20 iliyopita.

Askari Mzayuni akimkandamiza mtoto wa Kipalestina

Inaarifiwa kuwa, watoto zaidi ya 123 wa Kipalestina wameuawa shahidi huku wengine wengi wakijeruhiwa, tokea Rais anayeondoka wa Marekani, Donald Trump atoe tangazo tata la kuitambua Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel mnamo Disemba mwaka 2017.

Kadhalika watoto wengine 17,000 wa Kipalestina walikamatwa na kuzuiliwa katika mazingira ya kuogofya katika kipindi hicho kilichotajwa. Aidha zaidi ya watoto elfu saba wa Kipalestina wamekamatwa na polisi ya Israel tokea mwaka 2015.