Shirika la WFP: Yemen inajongewa na ukame mbaya zaidi wa karne
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ametahadharisha kuwa, Yemen inakaribia kukumbwa na ukame mbaya zaidi wa karne na kueleza kwamba, watu milioni 16 nchini humo wanataabika kwa njaa huku milioni tano kati yao wakikabiliwa na hatari ya kukumbwa na ukame.
David Beasley amezitaka pande zinazopinga nchini Yemen kusitisha vita ili kuzuia kupotea roho zaidi za wananchi wa nchi hiyo ambao wanakabiliwa na matatizo chungu nnzima.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ameashiria pia nakisi ya bajeti kwa ajili ya misaada ya kibinadamu na hatua ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia ya kuzuia kupelekwa matanki ya mafuta huko al-Hudaydah na kueleza kwamba, hizo ni baadhi ya sababu zinazopelekea hali ya wananchi hao kuzidi kuuwa mbaya.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ameonya kuwa, kama hakutachukuliwa hatua za haraka kuwasaidia wananchi hao, basi ulimwengu utashuhudia ukame mbaya zaidi wa karne katika nchi hiyo.
Hivi karibuni pia mashirika manne ya Umoja wa Mataifa ya Mpango wa Chakula WFP, Shirika la Chakula na Kilimo FAO, Shirika la Kuhudumia Watoto UNICEF na Shirika la Afya Duniani WHO, yalitangaza kuwa, katika mwaka huu wa 2021 kutakuwa na ongezeko la asilimia 22 la watoto wa umri chini ya miaka mitano watakaokabiliwa na hali mbaya sana ya lisheduni.
Ikumbukwe kuwa, kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa, mwezi Machi 2015 Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani.