Lebanon yaikosoa Israel kutumia anga yake kuishambulia Syria
Lebanon imekosoa vikali kitendo cha utawala wa Kizayuni wa Israel kutumia anga ya hiyo ya Kiarabu kutekeleza mashambulio ya makombora dhidi ya Syria.
Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon imesema inalaani kwa nguvu zote hatua ya utawala haramu wa Israel kutumia anga ya nchi hiyo Kiarabu katika mashambulio yake dhidi ya Syria.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, Lebanon inasimama pamoja na wananchi wa Syria ambao wanaandamwa kila uchao na mashambulio ya makomboya ya maadui.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon imesisitiza kuwa, hujuma hizo za anga za jeshi la utawala pandikizi la Israel mbali na kukanyaga haki ya kijitawala Lebanon, lakini pia zinakiuka sheria za kimataifa, Hati ya Umoja wa Mataifa na maazimio ya kimataifa.
Mara kwa mara, ardhi ya Syria imekuwa ikilengwa kwa makombora ya Wazayuni ambayo yanavurumishwa kutoka anga ya Lebanon au kutoka kwenye Miinuko ya Golan ya Syria.
Alfajiri ya Alkhamisi iliyopita, Jeshi la Anga la Syria lilifanikiwa kutungua makombora kadhaa kutoka Israel kabla hayajatua kusini mwa Damascus. Ndege za kijeshi za Israel zilizovurumisha akombora hayo zilijipenyeza Syria kupitia mpaka wa Lebanon.