Hassan Diab: Lebanon inakaribia kusambaratika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i69234-hassan_diab_lebanon_inakaribia_kusambaratika
Waziri Mkuu wa muda wa Lebanon amesema ana wasiwasi juu ya hatari ya kusambaratika nchi yake kutokana na migogoro mikubwa iliyojitokeza na ambayo haijaweza kutatuliwa, ukiwemo wa kuunda serikali mpya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 20, 2021 03:37 UTC
  • Hassan Diab: Lebanon inakaribia kusambaratika

Waziri Mkuu wa muda wa Lebanon amesema ana wasiwasi juu ya hatari ya kusambaratika nchi yake kutokana na migogoro mikubwa iliyojitokeza na ambayo haijaweza kutatuliwa, ukiwemo wa kuunda serikali mpya.

Hassan Diab, waziri mkuu wa serikali ya mshikizo ya Lebanon ameyasema hayo katika safari yake nchini Qatar na katika mazungumzo aliyofanya na viongozi wa nchi hiyo, ambapo sambamba na kuashiria migogoro iliyoshindwa kutatuliwa hadi sasa, amezitaka nchi za Kiarabu zisiiache mkono Lebanon.

Diab ameashiria jinsi Qatar ilivyosimama kidete na kuwa bega kwa bega na serikali ya Lebanon mnamo mwaka 2006 na kuisaidia nchi hiyo katika suala la kuyajenga upya maeneo yaliyoharibiwa na vita kufuatia uvamizi wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel na akasema, tunawapa indhari ndugu zetu Waarabu kwamba Lebanon inakabiliwa na hatari kubwa na sasa nchi hii haina uwezo tena wa kuhimili na kusubiri chochote.

Kabla ya hapo Hassan Diab alikuwa ameshatahadharisha kuhusu hali tata ya Lebanon katika kukabiliana na matatizo kadhaa, likiwemo la kushindikana kuundwa serikali na kutatuliwa mgogoro wa uchumi uliotokana na mripuko wa bandari ya Beirut.

Maandamano ya upinzani dhidi ya hali ya Lebanon yaliyogubikwa na machafuko

Tangu msimu wa joto wa mwaka uliopita, ulipotokea mripuko mkubwa na haribifu katika bandari ya Beirut, Lebanon haijawa na serikali na imekuwa ikiongozwa na serikali ya mshikizo ya wazri mkuu wa muda Hassan Diab, ambayo nayo pia ilijiuzulu kufuatia mripuko huo na kuongezeka mashinikizo dhidi yake.

Hatimaye mnamo Oktoba 22, 2020, Saad Hariri alikabidhiwa jukumu la kuunda serikali mpya, lakini hadi leo hajafanikiwa kuunda baraza jipya la mawaziri wa serikali hiyo.../