Safari ya Hassan Diab nchini Qatar; malengo na umuhimu wake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i69252-safari_ya_hassan_diab_nchini_qatar_malengo_na_umuhimu_wake
Hassan Diab, Waziri Mkuu wa serikali ya mshikizo ya Lebanon Jumapili ya juzi tarehe 18 Aprili aliwasili Doha, mji mkuu wa Qatar ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu ulipoanza mwaka huu wa 2021.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2021 06:25 UTC
  • Safari ya Hassan Diab nchini Qatar; malengo na umuhimu wake

Hassan Diab, Waziri Mkuu wa serikali ya mshikizo ya Lebanon Jumapili ya juzi tarehe 18 Aprili aliwasili Doha, mji mkuu wa Qatar ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu ulipoanza mwaka huu wa 2021.

Akiwa nchini humo Diab amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa nchi hiyo.

Hassan Diab amekuwa Waziri Mkuu wa muda wa Lebanon kuanzia Agosti mwaka jana (2020). Tangu Oktoba mwaka jana, Waziri Mkuu huyo wa Lebaon hajafanya safari nje ya nchi na safari yake hii huko Doha Qatar inahesabiwa kuwa safari yake ya kwanza nje ya nchi katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Safari yake ya mwisho nje ya nchi ilikuwa ile aliyoifanya nchini Kuwait Oktoba mwaka jana, ambapo alikwenda kushiriki shughuli ya mazishi ya aliyekuwa Amir wa nchi hiyo Sabah al-Ahmad al-Jabir al-Sabah.

Kwa maneno mengine ni kuwa, Hassan Adib hajafanya safari rasmi ya kisiasa nje ya nchi kwa muda wa miezi sita.

Saad al-Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon aliyepewa jukumu la kuunda serikali mpya

Hassan Diab amefanya safari nchini Qatar katika hali ambayo, Jumamosi iliyopita alitarajiwa kufanya safari nchini Iraq kwa ajili ya kutiliana saini na viongozi wa Baghdad mikataba kadhaa ya ushirikiano. Hata hivyo safari hiyo iliakhirishwa kutokana na mashinikizo ya madola ya kigeni kama Saudi Arabia na Imarati dhidi ya Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhimi. Mintarafu hiyo, safari ya Hassan Diab inadhihirisha mamlaka ya kujitawala Doha katika maamuzi yanayohusiana na siasa za nje za nchi hiyo.

Jambo jingine ni kuwa, kuanzia Agosti mwaka jana Lebanon kwa namna fulani imekuwa ikishuhudia sokomoko na mkwamno wa kisiasa. Awali Mustafa Adib alijiondoa katika mchakato wa kuunda serikali baada ya takribani mwezi mmoja tangu apewe jukumu hilo; na kisha Saad al-Hariri akapewa jukumu hilo ambapo tangu Oktoba mwaka jana naye hajafanikiwa kuunda serikali.

Aidha tukitupia jicho jinsi anga ya kisiasa ilivyo huko Lebanon, tunaona kuwa, hakuna mwelekeo wa kutia matumaini kuhusiana na kadhia ya kuundwa serikali nchini humo. Saad al-Hariri Waziri Mkuu aliyepewa jukumu la kuunda serikali nchini Lebanon, naye mwezi Februari mwaka huu alifanya safari huko Qatar ambako alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo.

Rais Michel Aoun wa Lebanon

Kwa hakika safari hii ya Hassan Diab nchini Qatar ina umuhimu mkubwa kutokana na nafasi iliyonayo nchi hiyo ya Qatar. Qatar ni nchi tajiri na imekuwa ikitumia wenzo wa fedha na misaada kwa ajili ya kujitafutia satuwa na ushawishi katika nchi za Kiarabu.

Kwa upande wa kuchumi kwa sasa Lebanon inakabiliwa na hali mbaya ambapo wananchi wa nchi hiyo wamekuwa wakiandamana mara kwa mara kulalamikia hali mbaya ya kifedha inayowakabili.

Kwa muktadha huo na kwa kuzingatia misimamo ya baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo la Asia Magharibi na vilevile madola makubwa ulimwenguni iliyo dhidi ya Hassan Diab, mwanasiasa huyu anafanya juhudi za kuomba msaada wa fedha kwa serikali ya Doha ili apunguze sehemu ya matatizo ya kifedha yanayoikabili Lebanon.

Katika fremu hiyo, Khidhr Talib, mshauri wa Hassan Diab amesema kuwa, katika safari hiyo ya Qatar Waziri Mkuu wa serikali ya mshikizo ya Lebanon amewabainisha viongozi wa Doha kuhusiana na hali ya sasa ya Lebabon pamoja na mazingira magumu ya kifedha, kijamii, kimaisha na kiuchumi wanayokabiliwa nayo wananchi wa nchi yake.

Hassan Diab, Waziri Mkuu wa serikali ya mshikizo ya Lebanon 

Talib ameashiria pia matumaini walionayo  viongozi wa Lebanon ya kupata msaada wa Qatar na kueleza kwamba, Doha daima imekuwa pamoja na wananchi wa Lebanon na hakuna wakati ambao ilisita au ilifanya ubakhili kuwasaidia wananchi wa Lebanon.

Mbali na hayo, Qatar ina historia ya kuwa mpatanishi aliyefanikiwa katika migogoro ya ndani ya Lebanon. Upatanishi wa migogoro ya eneo ni moja ya mikakati ya sera za kigeni za Qatar. Mwaka 2008 baada ya kushadidi mizozo na mivutano ya ndani nchini Lebanon, serikali ya Qatar ilichukua jukumu la kuwa mpatanishi wa mirengo ya ndani nchini humo, upapatnishi ambao hatimaye ulizaa matunda na kupelekea kufikia tamati mizozo hiyo.

Hivyo basi inaonekana kuwa, filihali pia Qatar inafanya jitihada za kuwa mpatanishi baina ya makundi, mirengo ya kisiasa na shakhsia mbalimbali wa Lebanon na kuwakurubisha pamoja ili kwa njia hiyo isaidie kuhitimisha mivutano ya kisiasa inayohusiana na mchakato wa kuundwa serikali mpya nchini humo.