Hizbullah: Ukombozi wa Quds umekaribia zaidi ya wakati wowote ule
(last modified Thu, 06 May 2021 12:45:15 GMT )
May 06, 2021 12:45 UTC
  • Hizbullah: Ukombozi wa Quds umekaribia zaidi ya wakati wowote ule

Mkuu wa Baraza Kuu la Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema ukombozi wa Quds tukufu umejongea wakati huu, kuliko wakati mwingine wowote ule.

Abdullah Safi al-Din ambaye pia ni mwakilishi wa Hizbullah mjini Tehran amesema hayo katika hotuba yake kwa Kongamano la Pili la Kimataifa la Quds Tukufu katika mji mtakatifu wa Qum, yapata kilomita 140 kusini mwa Tehran.

Ameeleza bayana kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel haufahamu lugha nyingine isipokuwa ya silaha na kwamba makundi ya muqawama yanapaswa kujiimarisha zaidi kwa ajili ya kukabiliana na Uzayuni.

Afisa huyo mwandamizi wa Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, "kadri maadui wanavyokula njama-ukiwemo Muamala wa Karne wenye lengo la kutaka kusahaulika kadhia ya Palestina- ndivyo azma ya Wapalestina ya kuikomboa Quds tukufu inapata nguvu zaidi.

Siku ya Kimataifa ya Quds inaadhimishwa kesho Ijumaa

Ameashiria mchango wa mashujaa wawili wa kupambana na ugaidi katika eneo, Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na aliyekuwa Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea Wananchi wa Iraq (Hashdu Shaabi), Abu Mahdi al-Muhandes na kubainisha kuwa: Mashahidi hao wawili walisabilia maisha yao yote kuunga mkono kadhia ya Palestina na ukombozi wa ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Wawili hao pamoja na wanamuqawama wenzao wanane waliuawa shahidi katika shambulio la kigaidi la Marekani mjini Baghdad, Iraq Januari mwaka 2020.