Mahakama ya Ulaya yakataa kusikiliza kesi ya mauaji ya Yassir Arafat
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71928-mahakama_ya_ulaya_yakataa_kusikiliza_kesi_ya_mauaji_ya_yassir_arafat
Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya (ECHR) imetupilia mbali faili la kutaka kuchunguzwa upya kifo cha kutatanisha cha Yasser Arafat, Rais wa zamani wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 03, 2021 02:44 UTC
  • Mahakama ya Ulaya yakataa kusikiliza kesi ya mauaji ya Yassir Arafat

Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya (ECHR) imetupilia mbali faili la kutaka kuchunguzwa upya kifo cha kutatanisha cha Yasser Arafat, Rais wa zamani wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Mjane na binti ya Arafat, Suha El Kodwa Arafat na Zahwa El Kodwa Arafat waliwasilisha faili hilo katika mahakama hiyo ya mjini Strasbourg, kaskazini mashariki mwa Ufaransa, mwaka 2017, baada ya mahakama moja ya Ufaransa kutupilia mbali shauri lao kwamba kiongozi huyo wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliuawa.

Mwaka 2012, Suha El Kodwa Arafat, mjane wa Arafat alifungua faili hilo la mauaji ya mumewe katika mahakama moja nchini Ufaransa, akisisitiza kuwa rais huyo wa zamani wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alipewa sumu kabla ya kufariki dunia katika hospitali ya kijeshi mjini Paris, mwaka 2004; ingawaje madaktari wa Ufaransa walidai kuwa aliaga dunia kutoka na kiharusi.

Yasser Arafat, Rais wa zamani wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aliaga dunia Novemba 11, mwaka  2004 katika hospitali moja mjini Paris,  kwenye mazingira ya kutatanisha, akiwa na umri wa miaka 74.

Arafat enzi za uhai wake akihutubu katika mkutano wa uchumi

Katika uamuzi wake siku ya Alkhamisi, Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya lilitupilia mbali faili lililowasilishwa na familia ya Arafat ikidai kwamba hawakuwasilisha vielelezo na ushahidi wenye mashiko.

Hata hivyo mjane na binti ya Arafat wanasisitiza kuwa, haki yao ya kusikilizwa kesi hiyo kwa njia ya uadilifu imekiukwa, na kwamba mahakama hiyo ya Ulaya imekataa kupokea ushahidi mpya wa mtaalamu, kuhusu kifo cha Arafat.