Mamluki wa Saudia na Imarati wazidi kutwangana kusini mwa Yemen
Televisheni ya al Alam imetangaza habari ya kupamba moto mapigano ya silaha nzito baina ya mamluki wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Saudi Arabia kusini mwa Yemen na kutoa mwanya wa kuzidi kujiimarisha magenge ya kigaidi.
Televisheni hiyo imetangaza kuwa, kuendelea mapigano baina ya wanamgambo wa Saudia na Imarati kumetoa fursa ya kuongezeka machafuko na kupata nguvu magenge ya kigaidi kama al Qaida na Daesh au ISIS kusini mwa Yemen.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapigano baina ya mamluki wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu katika eneo la Lawdar mkoani Abyan, kusini mwa Yemen yameongezeka sana katika hali ambayo kila upande unazidi kupeleka silaha nzito kwenye eneo hilo na kuushambulia kwa maneno makali upande wa pili kuwa ndio uliosababisha kuongezeka mapigano hayo.
Magenge ya kigaidi ya al Qaida na Daesh yanatumia fursa hiyo kusonga mbele katika maeneo tofauti ya mkoa wa Abyan, suala ambalo kwa namna yoyote ile madhara yake makubwa yanakwenda kwa wananchi wa kawaida wa Yemen.
Katika ripoti yake, mwandishi wa televisheni ya al Alam amesema kuwa, maeneo ya kusini mwa Yemen yanaelekea kutumbukia kwenye vita, machafuko na mizozo mibaya mno isiyodhibitika. Mikoa yote ya kusini mwa Yemen, kuanzia Aden hadi Lahij, Shabwah mpaka Abyan, kote huko kuna vita, machafuko na mapigano mapya baina ya wanamgambo wa Imarati na Saudi Arabia na kuongezeka harakati za magenge ya kigaidi ya al Qaida na Daesh (ISIS).
Tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa, muungano vamizi wa Yemen ambao wavamizi wake wakuu ni Saudi Arabia na Imarati, wamekuwa wakifanya jinai na ukatili usio na kifani dhidi ya wananchi Waislamu wa Yemen.