Saudi Leaks: Saudi Arabia imezidisha hukumu za kunyoga wapinzani na wanaharakati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i72020-saudi_leaks_saudi_arabia_imezidisha_hukumu_za_kunyoga_wapinzani_na_wanaharakati
Ripoti zinaonesha kuwa hukumu za kunyongwa watu zimeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini Saudi Arabia katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu wa 2021 ikilinganishwa na mwaka jana.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jul 05, 2021 04:54 UTC
  • Saudi Leaks: Saudi Arabia imezidisha hukumu za kunyoga wapinzani na wanaharakati

Ripoti zinaonesha kuwa hukumu za kunyongwa watu zimeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini Saudi Arabia katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu wa 2021 ikilinganishwa na mwaka jana.

Mtandao wa habari wa Saudi Leaks umefichua kuwa, katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu hukumu za kunyongwa watu wasiopungua 31 zimetekelezwa nchini Saudi Arabia na kwamba idadi hiyo ni mara mbili zaidi ya watu walionyongwa mwaka jana katika kipindi kama hicho. 

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Saudi Arabia wanasema mwaka jana utawala wa kizazi cha Aal Saud ulipunguza utoaji wa hukumu za kunyongwa wapinzani kwa shabaha ya kuboresha sura yake kimataifa, lakini adhabu ya kunyonga bado inatumiwa kama njia ya kuwanyamazisha na kuwakandamiza wapinzani na wakosoaji wa utawala huo. 

Utawala wa kifalme wa Saudi Arabia umekuwa ukiwahukumu kifo na kuwanyonga wafungwa wa kisiasa, wanaharakati na wapinzani kwa tuhuma zisizo na msingi kama ugaidi na kadhalika.

Jumuiya na mashirika mengi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanaendelea kukosoa hukumu ya kifo inayotolewa nchini Saudia dhidi ya wapinzani na wanaharakati wa masuala ya kijamii. Jumuiya hizo zinasisitiza kuwa, Saudi Arabia ni miongoni mwa tawala zinazoongoza duniani katika ukiukaji wa haki za binadamu.