Diab: Lebanon inakaribia kukumbwa na 'mlipuko wa kijamii'
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i72072-diab_lebanon_inakaribia_kukumbwa_na_'mlipuko_wa_kijamii'
Kaimu Waziri Mkuu wa Lebanon Hassan Diab ameonya kuwa nchi yake inakaribia kukumbwa na 'mlipuko wa kijamii' huku uchumi wa nchi hiyo ukiendelea kuzorota kutokana na mkwamo katika uundwaji wa serikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2021 23:03 UTC
  • Diab: Lebanon inakaribia kukumbwa na 'mlipuko wa kijamii'

Kaimu Waziri Mkuu wa Lebanon Hassan Diab ameonya kuwa nchi yake inakaribia kukumbwa na 'mlipuko wa kijamii' huku uchumi wa nchi hiyo ukiendelea kuzorota kutokana na mkwamo katika uundwaji wa serikali.

Akizungumza na mabalozi wa nchi za kigeni mjini Beirut Jumanne, Diab amesema zimesalia siku chache tu kabla ya Lebanon kukumbwa na mlipuko wa kijamii. Diab, ambaye anakaimu nafasi hiyo tokea alipojiuzulu mwezi Agosti mwaka jana kutokana na mlipuko katika bandari ya Beirut, ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuikosoa nchi yake wakati huu inapokabiliwa na mgogoro.

Lebanon ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa baada ya kutokea mlipuko huo mkubwa katika bandari ya Beirut. Mlipuko huo ulitokea tarehe nne Agosti mwaka jana na kusababisha vifo vya watu 190 na kujeruhi wengine 6,500.  Tokea wakati huo, makundi ya Lebanon yameshindwa kutatua hitilafu zao na kuunda serikali.

Benki ya Dunia inasema Lebanon inakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kiuchumu kuwahi kuikumba nchi yoyote katika karne. Sarafu ya Lebanon imepoteza asilimia 90 ya thamani yake tokea 2019 na zaidi ya nusu ya watu wa nchi hiyo wamepoteza ajira na biashara nyingi kufungwa. Pato Ghafi la Ndani la Taifa -GDP la nchi hiyo yenye watu milioni sita lilipungua kwa asilimia 40 na kufikia dola billioni 33 mwaka jana  kutoka dola bilioni 55 mwaka 2018.

Mlipuko wa Bandari ya Beirut

Janga la COVID-19 na mlipuko wa bandari ya Beirut ni matukio ambayo yamepelekea hali katika nchi hiyo kuwa mbaya zaidi.

Mwezi uliopita Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah, Sayyed Hassan Nasrallah, alisema njia pekee ya Lebanon kujikwamu katika mgogoro wa sasa ni kuunda serikali yenye uwezo wa kufanya kazi kwa ushirikiano baina ya waziri mkuu na rais.