Yemen: Marekani ndiyo inayoongoza moja kwa moja mashambulizi ya wavamizi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i72092-yemen_marekani_ndiyo_inayoongoza_moja_kwa_moja_mashambulizi_ya_wavamizi
Kaimu Mkuu wa Majeshi ya Yemen amesema kuwa, wanajeshi wa Marekani ndio wanaoongoza vita vinavyoendelea hivi sasa katika mkoa wa al Bayda' wakishirikiana na magaidi wa al Qaida, Daesh (ISIS) na Jabhat al Nusra.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 07, 2021 07:49 UTC
  • Yemen: Marekani ndiyo inayoongoza moja kwa moja mashambulizi ya wavamizi

Kaimu Mkuu wa Majeshi ya Yemen amesema kuwa, wanajeshi wa Marekani ndio wanaoongoza vita vinavyoendelea hivi sasa katika mkoa wa al Bayda' wakishirikiana na magaidi wa al Qaida, Daesh (ISIS) na Jabhat al Nusra.

Shirika la habari la SABA la Yemen limetangaza habari hiyo na kumnukuu Meja Jenerali Ali Hamud al Mushki, akifichua uhakika huo na kuongeza kuwa, wakati wanajeshi wa Marekani walipochukua jukumu la kuongoza vita dhidi ya wanajeshi wa Yemen katika mkoa wa al Bayda', wananchi na jeshi la Yemen limevunja jeuri na majigambo ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel wanaoongoza vibaraka na maluki wao kufanya jinai dhidi ya wananchi wa Yemen.

Meja Jenerali al Mushki vile vile amesema, wavamizi watatimuliwa wote katika ardhi ya Yemen na kipigo watakachopata ni kichungu sana kuliko walichopata wavamizi waliowatangulia hawa wa hivi sasa.

Wapiganaji wa Yemen

 

Taarifa zinasema kuwa, idadi kubwa ya magaidi wa ISIS, al Qaida na magenge mengine ya kigaidi wanaongozwa na wanajeshi wa Marekani katika mashambulizi ya maeneo mbalimbali ya Yemen hasa mkoa wa al Bayda'.

Baada ya wanajeshi wa madola vamizi yanayoongozwa na Saudi Arabia kushindwa vibaya katika mkoa wa Ma'rib, wavamizi hao na mamluki wao wameamua kutumia magenge ya kigaidi kama al Qaida, Daesh na Jabhat al Nusra kuanzisha medani mpya za vita katika mkoa wa al Bayda' ulioko umbali wa kilomita 209 mashariki mwa mji mkuu, San'a.