May 17, 2016 07:06 UTC
  • Ukiukaji wa kupindukia mipaka wa haki za binadamu nchini Bahrain

Ripoti ya jumuiya ya haki za binadamu ya Bahrain kuhusu uvunjwaji mkubwa wa haki binadamu nchini humo unaofanywa na utawala wa Aal Khalifa, kupasishwa hukumu ya kifungo cha maisha jela na mahakama kuu ya rufaa dhidi ya wapinzani wanne wa serikali na tamko la viongozi wa kidini wa Bahrain la kulaani siasa za ukoo wa kifalme wa nchi hiyo, ni miongoni mwa mambo muhimu yaliyogonga vichwa habari katika siku za hivi karibuni.

Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Bahrain imetangaza kuwa, wiki iliyopita yaani kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 13 Mei, kumeripotiwa kesi 25 za kutiwa mbaroni watu kiholela, kutekwa nyara watu 15, kufanyiwa ukatili watu 13 na miamala mibaya ya ukandamizaji vilivyofanywa na maafisa wa utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain. Taasisi hizo pia zimesisitiza kuwa, katika kipindi cha wiki hiyo, jumla ya hukumu 89 za kidhalimu zimetolewa ikiwa ni pamoja na hukumu dhidi ya raia 19 wa nchi hiyo, na wengine 18 kati ya 36 waliotiwa mbaroni kwa tuhuma za kushiriki maandamano ya amani dhidi ya serikali. Kadhalika watu 85 walihukumiwa kifungo cha muda mfupi au kuongezewa muda wa kuendelea kushikiliwa kupitia amri ya mwanasheria mkuu wa nchi hiyo. Wakati huo huo, taasisi hizo zimeripoti kushikiliwa watoto watatu katika uvamizi wa askari wa utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa dhidi ya nyumba za raia wa eneo la al-Ali nchini humo. Katika upande mwingine, habari zinaarifu kuwa, mahakama kuu ya rufaa nchini humo imeidhinisha adhabu ya kifungo cha maisha jela, dhidi ya watu wanne kwa tuhuma bandia za kuhusishwa na mashambulizi dhidi ya polisi wa nchi hiyo katika kijiji cha Diraz. Mwendesha mashitaka mkuu wa eneo la Diraz Ahmad al-Hamadi, amewahukumu kifungo hicho cha maisha jela vijana hao watatu kwa tuhuma za kubambikiziwa. Kwa mujibu wa tuhuma hizo bandia, vijana hao walihusika na vitendo vya kigaidi mji hapo. Kufuatia hukumu hiyo ya kidhalimu, viongozi wa kidini nchini Bahrain sanjari na kutoa ripoti ya kulaani siasa za ukandamizaji wa utawala huo wa kiukoo wa Aal-Khalifa, wametangaza kuwa, hivi sasa nchi hiyo inaongozwa na mfumo wa dhulma, ukandamizaji wa uhuru na sheria. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya wasomi hao wa kidini, baada ya utawala wa nchi hiyo kufanya ukandamizaji wa kidini, sasa unatumia ukandamizaji wa kisiasa na kufanya kila uwezalo ili kuwalazimisha wananchi wasiweze kuipinga serikali hiyo ya kidikteta nchini Bahrain. Kadhalika ripoti ya wanazuoni wa kidini nchini humo sanjari na kulaani uamuzi wa hivi karibuni wa utawala huo wa kupiga marufuku harakati za kisiasa za wasomi hao wa kidini, imesisitiza kuwa, kwenda kinyume na demokrasia na matukufu ya kibinaadamu na kuwalazimisha kukaa kimya wasomi hao wa dini, licha ya kutambua nafasi muhimu ya dini na kisiasa ya shakhsia hao, ni dhulma ya wazi dhidi ya nchi hiyo. Si vibaya kuashiria kuwa, Bahrain imekuwa ikishuhudia vitendo vya ukandamizaji mkubwa wa polisi tangu mwaka 2011, kufuatia kuongezeka malalamiko na maandamano ya amani ya wananchi yaliyoanza tarehe 14 Februari mwaka huo. Katika fremu hiyo, tarehe 14 mwezi Machi mwaka huo huo yaani ikiwa ni mwezi mmoja baada ya kuanza malalamiko ya wananchi, watawala wa Aal Saud nchini Saudi Arabia walituma askari wa nchi hiyo huko Bahrain kwa lengo la kuwakandamiza wananchi wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo kwa mara kadhaa taasisi za kimataifa kama vile Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International na mashirika ya haki za binaadamu, zimekuwa zikikosoa ukimya wa Umoja wa Mataifa jmbele ya ukandamizaji mkubwa unaofanywa na utawala wa Manama. Mfano wa wazi wa suala hilo ni namna Shirika la Human Rights Watch lilivyotoa ripoti hivi karibuni na kusema kuwa, mfumo wa mahakama nchini Bahrain ni wa kidhulma, kiukandamizaji na hauko huru.

Tags