Facebook yafungia shirika kubwa zaidi la habari la Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i72350-facebook_yafungia_shirika_kubwa_zaidi_la_habari_la_palestina
Kampuni ya Facebook ya Kimarekani imefunga ukurasa wa shirika kubwa zaidi la habari la Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2021 06:52 UTC
  • Facebook yafungia shirika kubwa zaidi la habari la Palestina

Kampuni ya Facebook ya Kimarekani imefunga ukurasa wa shirika kubwa zaidi la habari la Palestina.

Mkurugenzi wa shirika la habari la Shehab, Hisham al Zayegh amesema mtandao wa kijamii wa Facebook umefuta ukurasa wa shirika hilo kubwa zaidi la habari la Palestina na kwamba hatua hiyo inakiuka sheria za kimataifa na uhuru wa kusema na kujieleza.

Mkurugenzi wa shirika la habari la Shehab amelaani hatua hiyo na kusema Facebook inapinga na kupiga vita suala lolote linalotetea mapambano ya Palestina kwa kutumia visingizio eti vya ukiukaji wa kanuni na kuchochea machafuko.

Shirika la habari la Shehab la Palestina liliasisiwa mwaka 2007 na lina wafuasi milioni 7.5 katika mtandao wa jamii wa Facebook. 

Jumuiya ya Waandishi Habari wa Palestina pia imetoa taarifa ikilaani hatua hiyo ya Facebook. 

Mwaka 2018 Wizara ya Sheria ya Israel ilitangaza kuwa, kampuni ya Facebook mwaka 2017 ilifuta asilimia 85 ya mambo yote yaliyoandikwa katika mtandao huo wa kijamii kutokana na matakwa ya utawala huo na kwamba iliafiki kufuta au kufungia maandishi yote yanayohusiana na Palestina. 

Mwezi Mei mwaka huu pia mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram imechukua msimamo wa kuwaunga mkono wazayuni makaltili wa Israel kwa kufuta ujumbe, picha na filamu za waungaji mkono wa Palestina hasa makundi yanayotayarisha na kurusha hewani picha na filamu zilizoonyesha ukatili na mauaji yanayofanywa na Israel huko Palestina.

Watumiaji wa mitandano ya kijamii ya Facebook na Instagram wanasema, mitandao hiyo inachuja sana jumbe zote zinazotumwa katika kurasa zao ili kuzuia picha na filamu zinazofichua uhalifu na mauaji yanayofanywa na Israel huko Gaza na Quds tukufu.