Ripoti: Muungano vamizi wa Saudi Arabia umekiuka usitishaji vita mara 166
Chumba cha Operesheni cha Maafisa wa Jeshi la Yemen kimetangaza kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na utawala vamizi wa Saudi Arabia pamoja na mamluki wao umekiuka usitishaji vita huko al-Hudaydah mara 166.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, wavamizi wa Saudia pamoja na mamluki wao wamepaisha ndege 9 za kijasusi, wamefanya mashambulio ya mizinga mara kadhaa na kumimimina risasi mara 136 katika mkoa wa al-Hudaydah na hivyo kukiuka usishaji vita katika mkoa huo.
Jeshi la Yemen limelaani vikali hatua hiyo ya wanajeshi vamizi wa muungano unaoongozwa na Saudia ya kukiuka mara kwa mara usitishaji vita katika mkoa huo.
Usitishaji vita katika mkoa wa al-Hudaydha ulianza kutekelezwa Disemba 18 mwaka 2018 katika mkoa wa al-Hudaydah, hata hivyo muungano vamizi unaoongozwa na Sudi Arabia umekuwa ukikiuka kila siku usitishaji vita huo.
Saudi Arabia huku ikungwa mkono na Marekani na nchi nyingine kadhaa, Machi 25 mwaka 2015 zilianzisha hujuma na mashambulizi makubwa huko Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, angani na nchi kavu.
Vita hivyo vya kidhulma vya Saudia na waitifaki wake huko Yemen hadi sasa vimesababisha kuuliwa Wayemeni zaidi ya elfu 16, kujeruhiwa makumi ya maelfu na kuwa wakimbizi mamilioni ya wengine.
Aidha asasi na jumuiya mbalimbali za misaada ya kibinadamu zimetahadharisha mara chungu nzima kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili Yemen na hata uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo.