UN yalaani shambulio la kigaidi katika kitongoji cha Sadr, Baghdad, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i72638-un_yalaani_shambulio_la_kigaidi_katika_kitongoji_cha_sadr_baghdad_iraq
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani shambulio la kigaidi lililofanywa na genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS) katika kitongoji cha Sadr, mashariki mwa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jul 22, 2021 03:26 UTC
  • UN yalaani shambulio la kigaidi katika kitongoji cha Sadr, Baghdad, Iraq

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani shambulio la kigaidi lililofanywa na genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS) katika kitongoji cha Sadr, mashariki mwa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametoa taarifa ya pamoja na kulaani vikali shambulio la kiwoga la magaidi wa Daesh katika kitongoji cha Sadr, mjini Baghdad.

Katika taarifa yake hiyo, Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka kutolewe adhabu kali kwa wote waliofanya shambulio hilo, waliopanga shambulizi hilo na kila aliyesaidia kifedha na kwa namna yoyote ile. Baraza hilo limetaka kufuatiliwa wahusika wote wa kitendo hicho cha kinyama na cha aibu na kufikishwa kwenye vyombo vya mahakama.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

 

Kabla ya hapo, Katibu Mkuu wa harakati ya A'saaib Ahlil-Haq ya nchini Iraq, Qais Khazali, alikuwa ameashiria njama za Marekani za kutaka kuliimarisha genge la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) nchini Iraq na kusema kuwa, katika kufanikisha jambo hilo, Washington inasaidiwa na mashirika ya kijasusi ya Israel na nchi za Kiarabu.

Soko la al Wahilat lililoko kwenye kitongoji cha Sadr mashariki mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad, siku ya Jumatatu lilishuhudia mripuko mkubwa wa bomu lililotegwa na genge la kigaidi la DAESH (ISIS) ambao ulisababisha watu wasiopungua 300 kuuawa na wengine 60 kujeruhiwa.

Ijapokuwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limesambaratishwa nchini Iraq lakini baadhi ya wanachama wake wangaliko maeneo tofauti ya nchi hiyo wakifanya hujuma za kuvizia za kigaidi..