Malengo ya Imarati ya kuvikalia kwa mabavu visiwa vya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73960-malengo_ya_imarati_ya_kuvikalia_kwa_mabavu_visiwa_vya_yemen
Ahmed al-Rahwi mwakilishi wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen Jumanne wiki hii kwa mara nyingine tena aliutahadharisha Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kwamba, nchi hiyo itapewa somo na funzo iwapo haitaondoka katika kisiwa cha Mayyun.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 27, 2021 02:35 UTC
  • Malengo ya Imarati ya kuvikalia kwa mabavu visiwa vya Yemen

Ahmed al-Rahwi mwakilishi wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen Jumanne wiki hii kwa mara nyingine tena aliutahadharisha Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kwamba, nchi hiyo itapewa somo na funzo iwapo haitaondoka katika kisiwa cha Mayyun.

Kisiwa cha Mayyun au Perim kina umuhimu mkubwa kutokana na nafasi yake ya kistratejia na ndio maana kinakodolewa macho ya tamaa na madola mbalimbali yanayopenda kujitanua na kupenda makuu. Imarati na Saudi Arabia zimefanya kila ziwezalo kukidhibiti kisiwa hicho cha Yemen tangu mwezi Machi mwaka 2015 pale muungano vamizi unaoongozwa na Saudia ulipoivamia kijeshi ardhi ya Yemen. Moja ya sababu zinazoifanya Imarati iyaunge mkono na kuyakingia kifua makundi na wanamgambo mamluki wanaojiita Baraza la Mpito la Kusini ni kuandaa uwanja wa kuigawa Yemen ili hatimaye imiliki baadhi ya visiwa vya nchi hiyo kama Socotra na Mayyun. 

 Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kwa kushirikiana na Wazayuni, mwezi Disemba mwaka 2017 ulianzisha njama mbalimbali dhidi ya Yemen baada ya kuaga dunia Rais wa zamani wa nchi hiyo, Ali Abdallah Saleh kwa lengo la kuanzisha taasisi za kijeshi katika pwani ya magharibi mwa Yemen ukimtumia Tariq Saleh, mwana wa kiume wa kaka yake Ali Abdallah Saleh. Tangu wakati huo hadi sasa Imarati inatekeleza njama zake chafu huko kusini na magharibi mwa Yemen hususan katika visiwa vya nchi hiyo inavyovikalia kwa mabavu.

Rais wa zamani wa Yemen, Ali Abdallah Saleh 

Visiwa kama Socotra kinachopatikana katika Ghuba ya Aden kusini mwa Yemen na Mayyun au Perim katika lango bahari la Babul Mandab kusini magharibi mwa nchi hiyo, vinakodolewa jicho la tamaa na Imarati na utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na nafasi yake muhimu ya kijiografia. Iwapo visiwa viwili hivyo vitatwaliwa kwa mabavu hali hiyo itaandaa uwanja wa kudhibitiwa kikamilifu Ghuba ya Aden na lango bahari la Babul Mandab. Ndio maana Saudia ilianzisha uvamizi dhidi ya Yemen kwa kushirikiana na Imarati mwezi Machi mwaka 2015. 

Huku zikiungwa mkono na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, Saudia na Imarati zinafanya kila ziwezalo kuikalia kwa mabavu ardhi ya Yemen. Wakati huo huo wananchi na wanamapambano wa nchi hiyo wanatahadharisha kuwa, maghasibu na wale wote wanaotekeleza njama dhidi ya taifa la Yemen watajuta na kupewa darsa na funzo. Jumatatu wiki hii pia  Ahmed al-Rahwi mwakilishi wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen alitahadharisha kuwa adui mvamizi anapasa kupewa somo na funzo. 

Ukweli ni kuwa, Imarati na utawala wa Kizayuni wa Israel zinafanya jitihada za kutwaa visiwa viwili vya kimkakati huko Yemen yaani Socotra na Mayyun katika fremu ya kuimarisha uhusiano wao ili kwa njia hiyo zifanikiwa kudhibiti njia na vivuko vya majini vya kistratejia katika Bahari za Oman, Hindi na Bahari ya Arabu hadi huko Babul Mandal. Aidha lengo kuu la Imarati ni kuanzisha njama katika eneo la Magharibi mwa Asia hususan Ghuba ya Uajemi na kufanya njama na harakati za kijasusi dhidi ya baadhi ya nchi za Kiislamu katika eneo hilo. Hata hivyo viongozi wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen wamesisitiza mara kadhaa kwamba hatua za Imarati katika visiwa viwili hivyo zinakinzana na sheria za kimataifa na haziwezi kunyamaziwa kimya. Yemen imeionya Imarati kuwa, itatumbukia hatarini iwapo itaendeleza uvamizi wake katika ardhi ya nchi hiyo na kuvikalia kwa mabavu visiwa vyake 

Kisiwa cha Socotra huko Yemen