Iraq yaitaka Jordan imrejeshe nchini humo binti wa Saddam
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i7450-iraq_yaitaka_jordan_imrejeshe_nchini_humo_binti_wa_saddam
Serikali ya Iraq imeitaka Jordan imerejeshe nchini humo binti wa Saddam Hussein na wafuasi kadhaa wa karibu wa dikteta huyo wa Iraq wanaoishi nchini Jordan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 20, 2016 23:25 UTC
  • Iraq yaitaka Jordan imrejeshe nchini humo binti wa Saddam

Serikali ya Iraq imeitaka Jordan imerejeshe nchini humo binti wa Saddam Hussein na wafuasi kadhaa wa karibu wa dikteta huyo wa Iraq wanaoishi nchini Jordan.

Raghad Saddam Hussein, binti mkubwa wa Saddam amekuwa akiishi nchini Jordan alikokimbilia tangu mwaka 2003 wakati majeshi ya Marekani na Uingereza yalipoishambulia Iraq na kusababisha kung'olewa madarakani baba yake. Binti huyo wa dikteta wa zamani wa Iraq anaishi nchini Jordan kama 'mgeni wa familia ya kifalme' ya nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Ibrahim al-Jaafari aliwasilisha ombi hilo siku ya Jumatano baada ya balozi mdogo wa Jordan kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa Iraq katika mji wa Arbil.

Al-Jaafari amesema:"Iraq imeitaka Jordan iandae utaratibu unaohitajika kwa ajili ya kuwarejesha Iraq watu wanaoishi katika ardhi ya Jordan ambao wanatafutwa na vyombo vya mahakama vya Iraq".

Hadi sasa utawala wa kifalme wa Jordan umekataa kutekeleza ombi la Iraq la kumrejesha nchini humo Raghad Hussein mwenye umri wa miaka 47.

Serikali ya Iraq inataka kumfungulia mashtaka binti huyo wa Saddam kwa kuhusika na kufadhili kifedha vitendo na hujuma za kigaidi pamoja na kuyaunga mkono makundi ya wanamgambo wanaotaka kuiangusha serikali ya Iraq.

Raghad ambaye kutokana na kufanana mno na baba yake ni maarufu kwa jina la 'Saddam Mdogo' analiunga mkono bila ya kificho kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Mwaka 2010 Polisi ya Kimataifa Interpol ilitoa waranti wa kutiwa nguvuni Raghad kwa kufadhili kifedha makundi ya kigaidi nchini Iraq.

Serikali ya Iraq inataka pia kurejeshwa nchini humo maafisa wa chama cha Baath wanaoishi Jordan ambao wanatuhumiwa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi na kuhusika na utakatishaji pesa.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, maafisa wa jeshi la Iraq waliokuwa wakihudumu katika utawala wa Saddam Hussein wana nyadhifa za juu ndani ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ambalo tangu mwaka 2014 limekuwa likitenda jinai, hujuma na uharibifu mkubwa nchini Iraq.../