Oct 05, 2021 10:46 UTC
  • Serikali ya mamluki wa Saudia yawahukumu kifo maafisa wake kadhaa

Shirika la ujasusi wa kijeshi la serikali ya mamluki wa Saudi Arabia inayoongozwa na rais mkimbizi Abdu Rabuh Mansour Hadi, limewahukumu kifo maafisa wake kadhaa kwa kushindwa kuulinda mkoa wa Maarib.

Tovuti ya al Taghyir imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, baada ya jeshi la Yemen na kamati za kujitolea za wananchi wa nchi hiyo kupata ushindi mkubwa katika ukombozi wa mkoa wa Maarib, shirika la ujasusi wa kijeshi la serikali ya mamluki wa Saudia imeamua kumalizia hamaki zake kwa maafisa wake hasa baada ya wapiganaji wengi wa mamluki hao kujisalimisha kwa Jeshi na Answarullah.

Duru za kuaminika za kijeshi zimetangaza kuwa, lengo la serikali kibaraka ya Mansour Hadi ni kujaribu kuficha kipigo inachozidi kupata kutoka kwa wanamapambano wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen yenye makao yake mjini Sanaa.

Wanamapambano wa Ansarullah wakifurahia ushindi

 

Habari hiyo imesema kuwa, maafisa watano wa ngazi za juu wa jeshi la serikali ya Mansour Hadi wamehukumiwa kifo na mahakama ya kijeshi kwa kushindwa vibaya katika medani ya vita ya Sirwah.

Serikali hiyo ya mamluki wa Saudi Arabia imewahukumu kifo pia maafisa wengine kadhaa wa ngazi za chini kwa kushindwa kuzuia mashambulizi ya jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen ambazo hivi karibuni zimefanikiwa kukomboa maeneo muhimu sana ya kiistratijia ya mji wa Maarib wa mkoa Maarib wenye utajiri mkubwa wa maliasili yakiwemo mafuta na gesi.

Ikumbukwe pia kuwa, Jumamosi wiki hii, shirika la habari la Reuters, kitengo cha lugha ya Kiarabu lilizinukuu baadhi ya duru za kiusalama zikithibitisha habari ya kuzuka mapigano makali baina ya mamluki wa Imarati yalitokea Jumamosi asubuhi katika eneo la Crater mkoani Aden, kusini mwa Yemen.

Tags