Hamas yamkosoa rais wa FIFA kwa kuunga mkono utawala wa Israel
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestiina (Hamas) imesema hatua ya rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ya kushiriki katika ufunguzi wa jengo moja la makumbusho mjini Jerusalem (Quds) ambalo liko katika makaburi ya Wapalestina ni sawa na kuunga mkono uhasama wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Abdullatif al-Qanou, msemaji wa Hamas ametangaza Ijumaa kuwa, kushiriki Rais wa FIFA Giovanni Infantino katika ufunguzi wa jengo la makumbusho la Wazayuni ambalo limejengwa juu ya makaburi ya Kiislamu ya 'Ma'man Allah' mjini Quds ni sawa na kuupendelea utawala wa Kizayuni wa Israel na kupuuza masaibu ya Wapalestina. Aidha msemaji wa Hamas amesema kitendo hicho cha Infantino kitaupa kiburi zaidi utawala wa Kizayuni wa Israel uendeleze hujuma zake dhidi ya Wapalestina.
Al Qanou anasema rais wa FIFA amepuuza kanuni za shirikisho hilo za kutojihusisha na siasa sambamba na kutozingatia historia ya taifa la Palestina na turathi za kihistoria na kidini za mji wa Quds.
Msemaji wa Hamas amesisitiza kuwa, Makaburi ya Kiislamu ya 'Ma'man Allah' yalikuwa makaburi makubwa zaidi ya Kiislamu mjini Quds na ni dhihirisho la historia ndefu ya taifa la Palestina na matukufu yake.
Rais wa FIFA ametembelea utawala wa Israel na kushiriki katika ufunguzi wa jengo moja la makumbusho la Kizayuni mjini Quds, hatua ambayo inaendelea kulaaniwa vikali na Wapalestina na wapenda haki duniani.