Muqawama: Israel italipa gharama kubwa kwa uvamizi wowote dhidi ya Aqsa
(last modified Sat, 01 Jan 2022 02:59:47 GMT )
Jan 01, 2022 02:59 UTC
  • Muqawama: Israel italipa gharama kubwa kwa uvamizi wowote dhidi ya Aqsa

Makundi ya Muqawama ya Palestina yamesema luteka ya pamoja ya kijeshi iliyofanywa hivi karibuni na makundi ya mapambano ya Kiislamu katika Ukanda wa Gaza ilikuwa na ujumbe wa wazi kwamba, shambulio lolote dhidi ya Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa litapelekea Israel kulipa gharama kubwa.

Mohamed al-Barim, Msemaji wa Kamati za Muqawama za Palestina amesema mazoezi ya kijeshi yaliyofanyika hivi karibuni huko Gaza yalituma ujumbe wa tahadhari kwa Tel Aviv kwamba, iwapo Masjidul Aqsa itaharibiwa kivyovyote kutokana na chokochoko za utawala wa Kizayuni, basi makundi yote ya muqawama yatashirikiana katika kutoa jibu kali kwa wavamizi.

Katika mahojiano na shirika la habari la Shehab, al-Barim amesisitiza kuwa, wanamuqawama katu hawawezi kunyamazia kimya uchokozi wa Wazayuni, na kwamba daima watafanya juu chini kuhakikisha kuwa wafungwa wote wa Kipalestina wanaachiwa huru.

Msemaji wa Kamati za Muqawama za Palestina amebainisha kuwa, ujumbe mwingine wa mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza ni kuonesha utayarifu wa wanamuqawa katika kukabiliana na aina yoyote ya uchokozi wa wavamizi, mbali na kubadilishana mawazo.

Askari wa Kizayuni wakiihujumu Masjidul Aqsa

Kwa mujibu wa Ofisi ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Msikiti wa Al-Aqsa, walowezi zaidi ya 34,000 wa Kizayuni wamefanya mashambulizi dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa mwaka uliomalizika jana wa 2021.

Msikiti wa Al-Aqsa, ambaoni nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Palestina katika mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem), daima umekuwa ukilengwa kwa hujuma na vitendo vya uharibifu vya utawala ghasibu wa Israel na walowezi wa Kizayuni.