Khazali: Wanamuqawama wa Iraq watajibu uchokozi mpya wa Uturuki
-
Qais al-Khazali
Katibu Mkuu wa harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq ambalo ni tawi la muungano wa makundi ya muqawama wa Hashd al-Sha’abi nchini Iraq amesisitiza kuwa, mrengo wa mapambano ya Kiislamu utatoa jibu mwafaka kwa uvamizi na chokochoko mpya za jeshi la Uturuki dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Qais al-Khazali alitoa indhari hiyo jana Jumatano katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, "Serikali ya Ankara sasa imekwenda mbali zaidi kwa kuwalenga raia."
Amebainisha kuwa, kimya cha serikali ya Baghdad kwa hujuma za mara kwa mara za za jeshi la Uturuki lenye kambi zake kaskazini mwa Iraq kimeipa kiburi jeshi hilo vamizi.
Khazali amesisitiza kuwa, wanajihadi wa kambi ya muqawama nchini Iraq watatoa funzo kali kwa wanajeshi vamizi wa Uturuki.
Watu wasiopungua wanane waliuawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya ndege za kivita za Uturuki katika mji wa Sinjar kaskazini mwa Iraq.
Ndege hizo za kivita za Uturuki usiku wa kuamkia jana zililishambulia eneo la mlimani la Makhmour katika mkoa wa Nineveh kaskazini mwa Iraq kwa kisingizio cha kutaka kuwaangamiza wapiganaji wa PKK wa Kikurdi. Ankara inawatambua wapiganaji hao kama kundi la kigaidi.