Oxfam: Mapigano ya Ma'rib yamesababisha raia raia laki moja kuwa wakimbizi
Shirika la Kimataifa la Misaada kwa ajili ya Kupambana na Umaskini na Njaa (Oxfam) limetangaza kuwa, mapigano ya mwaka mmoja katika mji wa kistratejia wa Ma'rib huko Yemen yamesababisha watu karibu laki moja kuwa wakimbizi.
Saudi Arabia huku ikiungwa mkono na Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na nchi nyingine kadhaa waitifaki wake mwezi Machi mwaka 2015 ilianzisha mashambulizi huko Yemen na kuiwekea nchi hiyo maskini ya Kiarabu mzingiro wa baharini, nchi kavu na anga.
Vita vya Saudia na washirika wake vimebomoa zaidi ya asilimia 85 ya miundo mbinu ya nchi hiyo na kuisabababishia matatizo mbalimbali kama ukosefu mkubwa wa dawa na chakula.
Mohsen Sadiqi Mkurugenzi wa Oxfam nchini Yemen ameeleza kuwa, tahadhari hiyo inaonyesha namna vita vya Ma'rib vilivyoshadidisha hali mbaya ya kibinadamu kwa wakimbizi wa mkoa huo. Hii ni katika hali ambayo akthari ya wananchi wa Yemen wameikimbia nchi yao kutokana na vita na mapigano yanayoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Mkurugenzi wa Shirika la Oxfam huko Yemen ameongeza kuwa kwa akali muungano vamizi wa Saudia umetekeleza kwa akali mashambulizi ya anga 43 dhidi ya raia wa kawaida wa Yemen ikiwemo na kushambulia nyumba na mashamba yao katika mkoa wa Ma'rib katika mwezi Januari mwaka huu.