PLO yasimamisha uamuzi wa kuutambua utawala wa Kizayuni wa Israel
Baraza Kuu la Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO limetangaza kuwa limesimamisha uamuzi wa kuutambua utawala haramu wa Kizayuni wa Israel pamoja na ushirikiano wa kiusalama na utawala huo.
Baraza hilo la PLO limechukua uamuzi huo katika taarifa liliyotoa mwishoni mwa kikao chake cha 31 na kusisitiza kuwa, linasitisha kuutambua utawala wa Kizayuni pamoja na ahadi zote zilizoahidiwa kutekelezwa na serikali ya Mamlaka ya Ndani katika makubaliano iliyofikia na Tel Aviv, hadi itakapotambuliwa nchi huru ya Palestina kulingana na mipaka ya mwaka 1967.
Taarifa hiyo imesomwa na Azzam al Ahmad, mjumbe wa kamati ya utendaji ya PLO na kurushwa hewani na televisheni rasmi ya Palestina.
Wakati akisoma taarifa hiyo, Azzam al Ahmad amesema, Baraza Kuu la Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO, litasimamisha pia mashauriano yake yote ya kiusalama na Tel Aviv; na ili kuweka utaratibu mwafaka wa utekelezaji wa maamuzi hayo, kamati ya utendaji ya harakati hiyo imepewa jukumu la kuratibu utaratibu huo.
Wakati huohuo, Baraza Kuu la Palestina nalo pia limetangaza kuwa, limesimamisha uratibu na mashauriano ya aina yoyote ya kiusalama na utawala wa Kizayuni wa Israel.../