Jeshi la Yemen latungua ndege ya kijasusi katika mkoa wa Hajjah
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i80196-jeshi_la_yemen_latungua_ndege_ya_kijasusi_katika_mkoa_wa_hajjah
Vikosi vya Yemen vimefanikiwa kudungua ndege isiyo na rubani ya kijasusi ya muungano wa wavamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Hajjah.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2022 07:07 UTC
  • Jeshi la Yemen latungua ndege ya kijasusi katika mkoa wa Hajjah

Vikosi vya Yemen vimefanikiwa kudungua ndege isiyo na rubani ya kijasusi ya muungano wa wavamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Hajjah.

Katika taarifa iliyotolewa mapema Alhamisi, msemaji wa Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, amesema ndege hiyo ya kijasusi isiyo na rubani au drone iliangushwa na kombora la kutoka ardhini hadi angani katika anga ya wilaya ya Harad ya Hajjah.

Taarifa hiyo iliyochapishwa na mtandao wa televisheni wa al-Masirah wa Yemen imeongeza kuwa ndege hiyo ya kijasusi, aina ya CH-4 ilikuwa ikifanya vitendo vya uhasama kabla ya kudunguliwa.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Yemen, mapigano makali yanaendelea kati ya majeshi ya Yemen na wanamgambo wanaoungwa mkono na Saudi Arabia katika maeneo kati ya mkoa wa Hajjah na mpaka wa kusini mwa Saudi Arabia na kusababisha vifo na kujeruhi makumi ya watu wa pande zote mbili.

Msemaji wa Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree

Hivi karibuni Wizara ya Ulinzi ya Saudia ilitangaza kuwa imetuma brigedi mbili za kijeshi ndani ya ardhi ya Yemen ili kuanzisha operesheni kubwa yenye lengo la kuteka mikoa ya Sa'ada na Hajjah.

Makumi ya ndege zisizo na rubani za muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia zimetunguliwa na Jeshi la Yemen linaloshirikiana na kamati za wanachi za kujitolea vitani tangu Saudi Arabia ilipoanzisha uvamizi dhidi ya Yemen mwaka 2015.

Saudi Arabia inaungwa mkono kijeshi na Marekani katika uvamizi wake unaoendelea dhidi ya Yemen na ambao umepelekea makumu ya maelfu ya Wayemen kupoteza maisha, wengi wakiwa ni wanawake na watoto wasio na hatia.