Syria yalaani hujuma ya Israel dhidi ya Damascus
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i80200-syria_yalaani_hujuma_ya_israel_dhidi_ya_damascus
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imelaani vikali mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala haramu wa Israel dhidi ya maeneo ya Syria ambayo yamesababisha vifo na kujeruhi idadi kadhaa ya wanajeshi wa Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2022 07:20 UTC
  • Syria yalaani hujuma ya Israel dhidi ya Damascus

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imelaani vikali mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala haramu wa Israel dhidi ya maeneo ya Syria ambayo yamesababisha vifo na kujeruhi idadi kadhaa ya wanajeshi wa Syria.

Katika taarifa, wizara hiyo imesema mashambulizi hayo "yanajumuisha ukiukaji maradufu wa kanuni za sheria za kimataifa na zile za Mkataba wa Umoja wa Mataifa pamoja na maazimio muhimu kwa Lebanon na Syria."

Wizara hiyo imebainisha kuwa kimya cha jamii ya kimataifa na uungaji mkono wa Marekani umeupa kiburi utawala haramu wa Israel cha kuendelea na mashambulizi yake dhidi ya Syria.

"Serikali ya Syria inawaonya watawala wa taasisi ya Israel dhidi ya kuendelea ukiukaji wa wazi na wa kiholela wa Israel na mashambulizi ya jinai." Aidha Syria imeonya kuwa vitendo hivyo vya Israel vinaweza kuvuruga utulivu wa eneo na amani na usalama wa kimataifa.

Wizara hiyo pia imesisitiza kwamba mashambulizi ya "woga" yatakuwa na madhara makubwa kwa wahusika.

Taarifa hiyo pia imesisitiza haki ya Syria ya kutumia "njia zote halali" kujibu mashambulizi, na kuwawajibisha wale walio nyuma yake kuhusu "athari za hatari" za mashambulizi hayo.

Rais Bashar al Assad wa Syria

Mapema siku ya Jumatano, vikosi vya ulinzi wa anga vya Syria vilifanikiwa kuzuia na kutungua makombora yaliyorushwa na jeshi la Israel katika maeneo mbalimbali karibu na Damascus.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA, likinukuu chanzo cha kijeshi, liliripoti kwamba makombora kadhaa ya Israeli yalirushwa kutoka upande wa mji mkuu wa Lebanon wa Beirut katika maeneo fulani karibu na Damascus saa 00:56 asubuhi (2256 GMT Jumanne).

Utawala wa Kizayuni daima hulenga maeneo ya jeshi na miundombinu ya Syria katika kuwaunga mkono magaidi wanaoendesha mashambulizi kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar Asad wa nchi hiyo.