Lebanon yataka UN iishinikize Israel iache kukiuka anga yake
Jeshi la Lebanon limetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka kusitisha ukiukwaji wa anga yake unaotekelezwa mara kwa mara na utawala wa Kizayuni wa Israel wakati unaposhambulia nchi jirani ya Syria.
Katika mkutano baina ya Meja Jenerali Stefano Del Col Mkuu wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Mtaifa huko Lebanon (UNIFIL) na Brigedia Jenerali Haseb Abdo wa Jeshi la Lebanon, upande wa Lebanon umeutaka Umoja wa Mataifa uishinikize Israel isitishe uhasama wake hasa wa kutumia anga ya Lebanon wakati wa kushambulia kwa mabomu ardhi ya Syria. Katika kikao hicho cha Ijumaa kilichofanyika katika makao ya UNIFIL eneo la Ras Naqoura kusini mwa Lebanon, Brigedia Abdo pia ametaka Israel ikatazwe kwa ujumla kukiuka anga, bahari na nchi kavu ya Lebanon.
Jeshi la Lebanon limeonya kuhusu matokeo mabaya iwapo ndege za kivita za utawala wa Israel zitaendelea kukiuka anga ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Mara kwa mara, ardhi ya Syria imekuwa ikilengwa kwa makombora ya ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel ambayo yanavurumishwa kutoka anga ya Lebanon au kutoka kwenye Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Israel.
Wiki iliyopita Jeshi la Anga la Syria lilifanikiwa kutungua makombora kadhaa kutoka Israel kabla hayajatua Damascus. Ndege za kijeshi za Israel zilizovurumisha makombora hayo zilijipenyeza Syria kupitia mpaka wa Lebanon.