Vikosi vya Iraq vyaingia mji wa Fallujah na kuanza kuwatimua ISIS
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i8101-vikosi_vya_iraq_vyaingia_mji_wa_fallujah_na_kuanza_kuwatimua_isis
Wanajeshi wa Iraq Jumatatu wameingia katika mji wa Fallujah na kuanza kuwatimua magaidi wa ISIS au Daesh mjini humo katika hatua ambayo imetajwa kuwa ni ushindi mkubwa dhidi ya magaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2016 02:49 UTC
  • Vikosi vya Iraq vyaingia mji wa Fallujah na kuanza kuwatimua ISIS

Wanajeshi wa Iraq Jumatatu wameingia katika mji wa Fallujah na kuanza kuwatimua magaidi wa ISIS au Daesh mjini humo katika hatua ambayo imetajwa kuwa ni ushindi mkubwa dhidi ya magaidi.

Kamanda mwandamizi wa Iraq amenukuliwa akisema wanajeshi wa serikali wameingia Fallujah kutoka pande tatu katika awamu ya mwisho ya kuukomboa mji huo.

"Tulianza oparesheni zetu za kuingia Fallujah leo asubuhi," alisema Sabah al Norman, msemaji wa kikosi maalumu cha kupambana na ugaidi cha Iraq.

Mji wa Fallujah uko umbali wa maili 40 magharibi mwa mji mkuu Baghdad na ni moja ya ngome za mwisho za ISIS nchini Iraq.

Kundi hilo la Kitakfiri lingali linadhibiti maeneo ya kaskazini na magharibi, ikiwa ni pamoja na mji wa pili kwa ukubwa wa Iraq, Mosul.

Katika hotuba bungeni Jumapili, Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi ametoa wito kwa wakaazi wa Falluja kuondoka mjini humo au kubakia majumbani mwao.

Operesheni za kuukomboa mji wa Fallujah katika mkoa wa al-Anbar nchini Iraq zinazofanywa na jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na harakati za kujitolea za wananchi, zimepongezwa na makundi tofauti ya kisiasa na maraajii wakubwa wa taifa hilo. Hatua hiyo imekuja kufuatia mafanikio makubwa ya kuuzingira kikamilifu mji huo wa kistratijia.