Saudi Arabia yaruhusu tena ibada ya Umra kwa masharti
(last modified Sat, 12 Mar 2022 00:04:19 GMT )
Mar 12, 2022 00:04 UTC
  • Saudi Arabia yaruhusu tena ibada ya Umra kwa masharti

Serikali ya Saudi Arabia imewaruhusu Waislamu ambao hawajachanjwa dhidi ya virusi vya Corona, au ambao hawajakamilisha chanjo hiyo kufanya ibada ya Umra na kuingia Msikiti Mtakatifu wa Makka na Msikiti wa Mtume mjini Madina.

Ripoti zinasema, sasa kuna uwezekano kwa wageni wote wa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehma ambao hawajapata chanjo dhidi ya virusi vya corona au ambao hawakamilisha chanjo, kufanya ibada ya Umra na kuingia Masjidul Haram na Msikiti wa Mtume.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa: "Wageni wa Mwingi wa rehma wataruhusiwa kufanya ibada ya Umra na kuswali katika Misikiti Miwili Mitakatifu, kwa sharti kwamba hawana virusi vya corona na hawajasiliana na watu ambao wamethibitishwa kuwa na virusi hivyo."

Haya yanajiri baada ya tangazo la Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia, katika utekelezaji wa uamuzi wa kuondoa hatua za tahadhari katika Msikiti Mtukufu wa Makka na Msikiti wa Mtume mjini Madina.

Mwezi Machi mwaka 2020 Saudi Arabia iliwapiga marufuku raia wake na wakazi wa nchi hiyo kutekeleza ibada ya Umra katika mji wa Makka au kuzuru Msikiti wa Mtume (saw) katika mji wa Madina kwa hofu ya kuenea kirusi cha corona.

Mwishoni mwa mwaka huo Serikali ya Saudi Arabia imewaruhusu mahujaji kutoka nje kuingia nchini humo kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Umra baada ya kufungwa kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi Agosti mwaka jana Saudia ilikataa kupokea Waislamu kutoka nchi 33 duniani wakiwemo Wairani waliokusudia kuzuru Haramaini kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Umra.