Syria yawaachia huru mamia ya wafungwa
Wizara ya Sheria ya Syria imetangaza kuwa, serikali imewaachia huru mamia ya wafungwa waliokuwa wakituhumiwa kuwa na mfungamano na makundi ya kigaidi na kitakfiri na au kushiriki katika hujuma za kigaidi nchini humo.
Wizara ya Sheria ya Syria leo imetoa taarifa na kutangaza kuwa: wafungwa hao waliokuwa wakitoka katika mikoa mbalimbali ya Syria siku mbili zilizopitawameachiwa huru kwa mujibu wa dikrii ya msamaha namba 7 wa Rais Bashar al Assad kuhusu hujuma za kigaidi.
Taarifa ya Wizara ya Sheria ya Syria imeongeza kuwa, kwa mujibu wa ushirikiano kati ya Mahakama Maalumu inayoshughulikia hujuma za kigaidi na Mwendesha Mashtaka; hatua za lazima zinafanywa ili kuwaachia huru wafungwa zaidi walioko jela na wale ambao hukumu zao zimekiukwa.
Wizara hiyo imesisitiza kuwa, wafungwa wote walio chini ya msamaha wa Rais wataachiliwa huru kwa utaratibu katika siku zijazo.
Rais Bashar al Assad wa Syria Jumamosi Aprili 30 alitoa dikrii ya msamaha wa wote kwa watu waliokuwa wamefungwa jela wakituhumiwa kwa makosa na kuhusika katika vitendo vya ugaidi. Hata hivyo msamaha huu haujumuishi wale ambao matendo yao yamesababisha vifo vya watu.