Rais Bashar al-Assad: Ushindi wa Palestina ni ushindi wa Syria
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kuwa, ushindi wa kadhia ya Palestina ni ushindi wa Syria na kwamba, huu ndio msimamo wa serikali ya Damascus.
Rais wa Syria amesema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo mjini Damascus mji mkuu wa Syria na wajumbe wa Jumuiya ya Wapalestina wanaoishi barani Ulaya na kubainisha kwamba, uhusiano wa Syria na kadhia ya Palestina ni imara mno na hauishii tu katika mipaka ya kijiografia na kiitikadi.
Rais Assad ameeleza kuwa, uhusiano huo haujajengeka juu ya misingi ya maslahi kwani ushindi wa taifa la Palestina unahesabiwa kuwa ni ushindi wa taifa la Syria.
Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake na wajumbe wa Jumuiya ya Wapalestina wanaoishi nje ya nchi ambao wapo nchini Syria kushiriki kongamano lao la tano, Rais Assad amesema kuwa, hii leo kwa juhudi za Wapalestina watiifu walioko nje, kadhia ya Palestina inatambulika kimataifa na kadhia hii ni mdaiwa wa muqawama wa ndani na welewa wa kizazi kipya cha Palestina.
Rais wa Syria amewaambia wajumbe hao kuwa, nukta muhimu katika harakati za Wapalestina walioko nje ya nchi ni kufichua uongo ambao unataka kuwatambulisha wananchi wa Wapalestina kuwa ni magaidi.
Hili ni jambo ambalo wahusika wanapaswa kulifanya kwa nguvu zao zote na bila kuchoka, amesisitiza Rais Bashar al-Assad wa Syria.
Kwa upande wao wajumbe wa Jumuiya ya Wapalestina wanaoishi nje ya nchi wamesisitiza kuwa, mafanikio ya kongamno hilo yanatokana na himaya na uungaji mkono wa kweli wa Syria kwa kadhia ya Palestina.