Ansarullah: Kumvunjia heshima Mtume SAW ni kufilisika kimaadili
Msemaji wa Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, kumvunjia heshima Bwana Mtume SAW ni ishara ya wazi ya kufilisika kimaadili.
Muhammad Abdul-Salam, msemaji wa Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesema hayo katika radiamali yake kwa kitendo cha kifidhuli cha msemaji wa chama tawala nchini India cha kumvunjia heshima mbora wa viumbe Mtume Muhammad SAW na kubainisha kwamba, nafasi na cheo cha Mtume pamoja na risala yake ni mambo ya kuheshimiwa na wanadamu wote.
Ameongeza kuwa, Harakati ya Ansarullah inalaani vikali kitendo hicho na inakitambua kwamba, si kitu cha kukubalika hata kidogo.
Katika mdahalo wa televisheni, msemaji wa chama tawala cha India, BJP, Nupur Sharma alitoa matamshi ya kichochezi dhidi ya Mtume wa Uislamu, ambayo yamelaaniwa kote India na kuibua ghasia nchini humo. Jana Jumapili chama cha BJP kilitangaza kusimamisha uanachama wa Sharma na kujiweka mbali na matamshi yake yenye chuki.
Aidha chama hicho kimemfukuza kazi Naveen Kumar Jindal ambaye anasimamia kitengo cha habari cha chama hicho mjini New Delhi ambaye pia alituma ujumbe uliomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW katika ukurasa wake wa Twitter na kufuatia malalamiko alifuta ujumbe huo.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa taarifa na kulaani vikali matamshi hayo ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na kusema yamekuja huku kukishuhudiwa kuongezeka chuki na uhasama dhidi ya Uislamu nchini India na ukandamizaji dhidi ya Waislamu nchini humo.