Mfalme wa Saudia aibembeleza Qatar iimarishe uhusiano na Riyadh
Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz amemuandikia barua Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani akiiomba Doha ichukue hatua za kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Riyadh.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Qatar QNA, ujumbe huo wa maandishi wa Mfalme wa Saudia umekabidhiwa Amir wa Qatar na Balozi wa Saudia, Mwanamfalme Mansour bin Khalid bin Farhan.
Tokea Januari mwaka jana 2020 baada ya Saudia kuiangukia miguuni Qatar katika mji wa al-Ula na kuhuisha uhusiano wa pande mbili uliokuwa umeingia doa kwa zaidi ya miaka minne, Riyadh imekuwa ikifanya jitihada za kuboresha uhusiano wake wa Doha.
Ikumbukwe kuwa tarehe 5 Juni mwaka 2017, Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zilichukua hatua ya kuvunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa sababu ya serikali ya Doha kutofuata muelekeo wa nchi za Kiarabu zinazoongozwa na Saudia.
Lakini mbali na kuiwekea vikwazo Qatar, nchi hizo wanachama wa Baraza la Ghuba ya Uajemi zilifungia pia Doha mipaka yao ya ardhini, baharini na angani.
Qatar ilisimama kidete katika kipindi chote cha vikwazo, kutengwa na mzingiro wa kila upande wa nchi hizo za Kiarabu, huku ikiungwa mkono na kupewa msaada wa kibinadamu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.