Wabunge Lebanon washindwa tena kumchagua Rais
Bunge la Lebanon lilikutana tena jana (Jumatatu) na kwa mara nyingine likashindwa kumchagua Rais kutokana na kutotimia idadi ya mahudhurio ya Wabunge kwa ajili ya zoezi hilo.
Bunge hilo lililazimika kuakhirisha kikao chake cha kumchagua Rais wa nchi hii ikiwa ni mara ya 35 na hivyo kukifanya kiti cha rais kuendelea kuwa kitupu.
Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri alilazimika kuakhirisha kikao hicho na kutangaza tarehe tatu ya mwezi ujao wa Machi kuwa siku ya kukutana Bunge hilo kwa ajili ya zoezi la kumchagua Rais. Ni Wabunge 58 tu kati ya 128 wa Bunge la nchi hiyo ndio waliohudhuria kikao cha ljana. Ili Bunge la Lebanon liweze kumchagua Rais inabidi idadi ya Wabunge waliohudhuria kikao itimie theluthi mbili yaani Wabunge 86 kati ya Wabunge 128. Muhula wa uongozi wa Rais Michel Suleiman ulimalizika mwezi Mei mwaka juzi na hadi leo Bunge la nchi hiyo limeshindwa kumchagua Rais mpya. Kila mara bunge hilo limekuwa likishindwa kumchagua Rais kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kutotimia idadi ya Wabunge wanaohudhuria kikao. Rais wa Lebanon anapaswa kuchaguliwa miongoni mwa wagombea wa jamii ya Wakristo wa Maroni.