Wafungwa wa Palestina waanza mgomo wa kula
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i87306-wafungwa_wa_palestina_waanza_mgomo_wa_kula
Mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel wameanzisha mgomo usio na kikomo wa kula chakula.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Aug 22, 2022 06:37 UTC
  • Wafungwa wa Palestina waanza mgomo wa kula

Mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel wameanzisha mgomo usio na kikomo wa kula chakula.

Shirika la habari la Palestin al-Yaum limeinukuu Bodi ya Wafungwa Wapalestina ikisema kuwa, hali ya taharuki imetanda katika jela na magereza ya utawala wa Kizayuni, baada ya mateka hao wa Kipalestina kuanza mgomo wa chakula leo Jumatatu.

Kamati Kuu ya Dharura ya Wafungwa wa Kipalestina imetangaza kuwa, mgomo huo wa kula unaanza leo Jumatatu na kundi jingine la wafungwa litaanza Jumatano, kabla ya kuzinduliwa katika magereza na jela zote za Wazayuni wanakoshikiliwa kidhulma Wapalestina.

Mgomo huo wa kula ni muendelezo wa hatua za wafungwa wa Kipalestina, ambao wanalalamikia hali mbaya ya kibinadamu katika jela hizo za Wazayuni. Mateka zaidi ya 500 wa Kipalestina wamekataa kwenda kusikiliza kesi dhidi yao katika mahakama za kijeshi za Israel, tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.

Wafungwa wa Kipalestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel unatekeleza siasa za mauaji ya taratibu dhidi ya wafungwa wa Kipalestina kwa kutowapa matibabu ya dharura wanapokuwa katika jela zake.

Ukandamizaji dhidi ya Wapalestina ni wa kiwango cha juu sana. Wapalestina wanaotekwa nyara na wanajeshi makatili wa Israel hupewa mateso makubwa katika jela za kutisha za utawala huo pandikizi. Inakadiriwa kuwa, hivi sasa kuna Wapalestina 5,700 wanaoshikiliwa mateka katika jela za utawala wa Kizayuni.