Wafungwa 1,000 wa Kipalestina watishia kuanza mgomo wa kula
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i87576-wafungwa_1_000_wa_kipalestina_watishia_kuanza_mgomo_wa_kula
Wafungwa zaidi ya 1,000 wanaoshikiliwa katika jela na magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel wameonya kuwa wataanza mgomo wa kula chakula kulalamikia kukanyagwa kwa haki zao na ukandamizaji.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 30, 2022 02:32 UTC
  • Wafungwa 1,000 wa Kipalestina watishia kuanza mgomo wa kula

Wafungwa zaidi ya 1,000 wanaoshikiliwa katika jela na magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel wameonya kuwa wataanza mgomo wa kula chakula kulalamikia kukanyagwa kwa haki zao na ukandamizaji.

Kamati Kuu ya Wafungwa wa Kipalestina imesema, wafungwa wapatao 1,000 wa Kipalestina wataanza mgomo wa kula kuanzia Septemba Mosi katika awamu ya kwanza, kisha wengine watajiunga nao baadaye.

Taarifa ya kamati hiyo imesisitiza kuwa, mateka hao wa Kipalestina wanaoteswa na kunyongeshwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wataendelea na mgomo wao hadi pale matakwa yao yatakapotekelezwa.

Agosti 22, mateka wengine wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za kuogofya za utawala wa Kizayuni wa Israel walianzisha mgomo usio na kikomo wa kula chakula wakilalamikia hatua za kidhalimu na maafisa wa utawala huo katika magereza.

Mfungwa wa Kipalestina aliyedhoofika kutokana na mgomo wa kula

Zaidi ya wafungwa 7,000 wa Kipalestina kwa sasa wanazuiliwa katika takriban jela 17 za Israel. Mamia ya wafungwa, wakiwemo wanawake na watoto wadogo, wanazuiliwa bila kufunguliwa mashtaka hatua ambayo imelaaniwa vikali na makundi ya kutetea haki za binadamu.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, utawala haramu wa Israel umewatia mbaroni zaidi ya wanawake 16,000 wa Kipalestina tangu mwaka 1967 huku mashirika ya haki za binadamu yakionya kuhusu hali mbaya ya wafungwa wa kike katika jela za kuogofya za Israel.