Kinara wa ISIS, Abu Bakr Baghdadi, ajeruhiwa vitani Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i8899-kinara_wa_isis_abu_bakr_baghdadi_ajeruhiwa_vitani_iraq
Duru nchini Iraq zinadokeza kuwa kinara wa kundi la kigiaid la ISIS (Daesh), Ibrahim al-Samarrai, maarufu kama Abu Bakr al-Bahgdadi, amejeruhiwa katika hujuma ya ndege za kivita.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 10, 2016 14:11 UTC
  • Kinara wa ISIS, Abu Bakr Baghdadi, ajeruhiwa  vitani Iraq

Duru nchini Iraq zinadokeza kuwa kinara wa kundi la kigiaid la ISIS (Daesh), Ibrahim al-Samarrai, maarufu kama Abu Bakr al-Bahgdadi, amejeruhiwa katika hujuma ya ndege za kivita.

Televisheni ya Al Sumaria ya Iraq imenukulu duru katika mkoa wa kaskazini mwa nchi wa Ninevah zikisema kuwa kuwa Baghdadi na makamanda wengine wa kundi hilo la wakufurishaji walijeruhiwa siku ya Alhamisi magharibi mwa mkoa wa Ninevah, karibu na mpaka wa Syria.

Televisheni hiyo imeongeza kuwa al-Baghdadi, ambaye alikuwa anaaminika yuko katika ngome ya ISIS mjini Raqqah Syria, alijeruhiwa kufuatia bomu lililodondoshwa na ndege za waitifaki.

Oktoba mwaka jana pia kulikuwa na ripoti kuwa al-Baghdadi alijeruhiwa katika hujuma ya Jeshi la Anga la Iraq.

Jeshi la Iraq lilisema kuwa, kikosi chake cha anga kilishambulia msafara wa al-Baghdadi ambaye pia alikuwa anaaminika kuwa katika mkoa wa Anbar ulioko magharibi mwa nchi hiyo.

Al-Baghdadi alijitangaza kuwa mkuu wa kundi hilo la ISIS mwaka 2014 wakati kundi hilo lilipoyadhibiti maeneo mengi ya Iraq na Syria. Hata hivyo katika miezi ya hivi karibuni magaidi wa ISIS wamepata pigo kubwa sana katika nchi hizo mbili ambapo wanajeshi wa nchi hizo wanaendelea kukomboa ardhi zilizokuwa zimetekwa na kundi hilo la kigaidi.