Hizbullah: Saudia na Marekani zinakwamisha uchaguzi wa Rais wa Lebanon
(last modified Tue, 25 Oct 2022 10:59:54 GMT )
Oct 25, 2022 10:59 UTC
  • Hizbullah: Saudia na Marekani zinakwamisha uchaguzi wa Rais wa Lebanon

Afisa mwandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema balozi za Saudi Arabia na Marekani jijini Beirut zimekula njama na kuweka vizingiti vya kila aina ili kukwamisha uchaguzi wa rais, huku ikiwa imesalia wiki moja tu kabla ya kumalizika muhula wa Rais Michel Aoun wa nchi hiyo.

Sheikh Nabil Qaouk, Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Hizbullah amesema, "Si siri tena kwa taifa la Lebanon kwamba ubalozi wa Saudia unaingilia uchaguzi wa kumtafuta rais mpya, kama ulivyofanya katika uchaguzi wa Bunge la Lebanon (Mei 15)."

Amesema balozi za Marekani na Saudi Arabia mjini Beirut zinaingilia moja moja mchakato wa uchaguzi wa rais wa Lebanon na kuwawekea mashinikizo makubwa wabunge wa nchi hiyo ya Kiarabu ili kukwamisha zoezi hilo.

Sheikh Qaouk ameeleza bayana kuwa, uingiliaji huo wa Washington na Riyadh katika uchaguzi wa rais wa Lebanon hautakuwa na matokeo mengine isipokuwa kuufanya kuwa mgumu mchakato wa uchaguzi wenyewe na kuibua mipasuko miongoni mwa wagombea wanaochuana kurithi mikoba ya Rais Michel Aoun.  

Bunge la Lebanon

Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Hizbullah ameeleza kuwa, mabalozi wa Saudia na Marekani pamoja na vibaraka wao wanafanya juu chini kuhakikisha kuwa Lebanon inapata rais ambaye ataishinikiza harakati hiyo ya muqawama.

Matamshi ya afisa huyo mwandamizi wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon yametolewa baada ya Lebanon siku ya Jumatatu kushindwa tena kumchagua rais mpya wa nchi hiyo, kwa mara ya nne sasa.

 

Tags