Jun 14, 2016 02:28 UTC
  • Kushadidishwa ukandamizaji wa utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wananchi

Mfalme wa Bahrain amepiga marufuku shughuli za kisiasa za wanazuoni nchini humo lengo likiwa ni kushadidisha ukandamizaji kwa malalamiko ya raia wa nchi hiyo.

Sheikh Hamad bin Issa Aal Khalifa Mfalme wa Bahrain siku ya Jumapili alitoa dikrii na kubadili baadhi ya vipengee vya sheria ya nchi hiyo kuhusu vyama vya kisiasa na kuvipiga marufuku vituo vya kidini na wanazuoni nchini humo kuendesha shughuli za kisiasa.

Kwa mujibu wa dikrii hiyo, ni marufuku kutumiwa mimbari za kidini kutoa hotuba za kisiasa na pia ni marufuku kwa wakuu wa vituo vya kidini kuwa na uhusiano na vyama vya kisiasa nchini humo.

Vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Khalifa vimewatia mbaroni maulamaa wengi kwa sababu tu ya kuzungumzia masuala ya kisaisa katika hotuba za Swala za Ijumaa huko Bahrain. Wanajeshi wa Bahrain pia jana usiku waliivamia nyumba ya Nabil Rajab Mkuu wa Kituo cha Haki za Binadamu cha Bahrain na kumtia nguvuni. Wanajeshi wa utawala wa Aal Khalifa wanawakamata na kisha kuwasweka jela wanaharakati wa kisiasa wa Bahrain ili kukandamiza malalamiko ya amani ya wananchi. Itakumbukwa kuwa Bi Zainab al Khawaja mwanaharakati wa haki za binadamu wa huko Bahrain pia alilazimika kuondoka nchini humo mara baada ya kuachiwa huru kutoka katika jela za utawala wa Aal Khalifa. Bi Zainab al Khawaja alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu na mwezi mmoja jela na mahakama moja ya Bahrain. Katika kuendeleza ukiukaji wake wa haki za raia wa Bahrain, utawala wa Aal Khalifa ulifuta pia uraia wa wanachama watatu wa gadi ya taifa ya nchi hiyo. Naye Rashid bin Abdallah Aal Khalifa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Bahrain aliagiza kufungwa kamera na vifaa vya kiusalama katika taasisi zote za elimu, biashara, masuala ya hisani na hata katika nyumba za raia; yote hayo ikiwa ni katika kuendelezwa siasa za ukandamizaji na za kipolisi za utawala wa Aal Khalifa dhidi ya raia wa nchi hiyo.

Hii ni katika hali ambayo baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Bahrain pia yametoa radiamali yao kwa hatua za ukandamizaji za utawala wa Aal Khalifa na kuonyesha mshikamano wao na vijana wanamapinduzi wa Bahrain katika mapambano yao dhidi ya vitendo vya mabavu vya viongozi wa Bahrain dhidi ya wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo.

Duru za habari zimearifu kuwa Bahrain ambayo inapatikana katika eneo la Mashariki ya Kati magharibi mwa Asia ni nchi ya kwanza kwa kuwa na wafungwa wengi katika jela zake. Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa watu zaidi ya elfu nne wamefungwa jela Bahrain kwa kosa la kulalamikia na kufanya maandamano ya amani kupinga siasa za kibaguzi na ukandamizaji za utawala ulioko madarakani. Kati ya wafungwa wote wa nchi hiyo, wafungwa ambao wanasubiri kuhukumiwa ni asilimia 27, huku asilimia nne wakiwa ni wanawake na asilimia 2 ni watoto. Bahrain tangu mwaka 2011 imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya raia wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa Aal Khalifa. Wananchi wa Bahrain wanataka kuwa huru, uadilifu, kukomeshwa vitendo vya ubaguzi na kuingia madarakanii serikali ya kidemokrasia itakayochaguliwa na wananchi.

Tags