Walowezi wa Kizayuni waendeleza vitendo vya kuuvamia msikiti wa al-Aqswa
Makumi ya walowezi wa Kizayuni wameuvamia tena Msikiti wa al-Aqswa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu.
Mashuhuda wanasema kwamba, uvamizi wa walowezi hao wenye itikadi kali ulifanyika chini ya ulinzi mkali kutoka kwa wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel kupitia upande wa Babul al-Magharibah.
Walowezi hao wa Kizayuni wakisaidiwa na kupewa himaya na jeshi la Israel baada ya kuingia katika eneo la ndani la msikiti huo mtakatifu walisikika wakipiga nara dhidi ya Uislamu na Waislamu na kufanya vitendo vya kuchochea hisia za Waislamu.
Sambamba na uvamizi huo, wanajeshi wa Israel waliwazuia Waislamu kuingia katika eneo hilo ambao kimsingi walienda kutekeleza ibada ya Swala katika msikiti huo mtakatifu, kibla cha kwanza cha Waislamu.
Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno sambamba na njama za kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa eneo hilo takatifu.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.
Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.