Iran yalaani mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i94924-iran_yalaani_mashambulizi_ya_kinyama_ya_israel_dhidi_ya_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani wimbi la mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria, wakati huu ambapo taifa hilo linakabiliwa na matatizo chungu nzima kutoka na maafa makubwa ya matetemeko ya ardhi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 09, 2023 23:26 UTC
  • Iran yalaani mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani wimbi la mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria, wakati huu ambapo taifa hilo linakabiliwa na matatizo chungu nzima kutoka na maafa makubwa ya matetemeko ya ardhi.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika mazungumzo yake na Rais Bashar al-Assad wa Syria mjini Damascus jana Alkhamisi kwamba, mashambulizi hayo ya Wazayuni yanakinzana waziwazi na sheria za kimataifa kuhusu masuala ya kibinadamu na wakati huo huo yanauweka hatarini usalama na amani ya kikanda na kimataifa.

Amesema inasikitisha kuona Israel imechukua hatua ya kuzidisha na kushadidisha machungu na masaibu yaliyowafika watu wa Syria, ambao wakati huu wanakabiliwa na athari mbaya za matetemeko ya ardhi yaliyoua maelfu ya watu, mbali na kuharibu sehemu kubwa ya miundomsingi ya nchi hiyo.

Amesisitiza kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapasa kuushinikiza utawala wa Kizayuni ili uhitimishe chokochoko na hatua zake za uvamizi dhidi ya mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Syria.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran sambamba na kulipa pole taifa hilo kufuatia janga la mitetemeko ya ardhi ya karibuni, ameeleza kuwa, inasikitisha kuona jamii ya Kimataifa ingali inaendelea kunyamazia kimya jinai na unyama huo wa Wazayuni

Rais Assad akimpokea mgeni wake Waziri Abdollahian

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuna udharura wa kuondolewa vikwazo na mzingiro uliowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya taifa hilo la Kiarabu.

Katika mazungumzo hayo ya jana mjini Damascus, Rais Bashar al-Assad wa Syria kwa upande wake ametoa shukrani kwa jumbe za mkono wa pole za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei na Rais Ebrahim Raisi wa Iran, pamoja na misaada ya kibinadamu iliyotumwa na Wairani kwa ndugu zao wa Syria.

Amemshukuru Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran kwa kuitembelea nchi hiyo iliyokumbwa na janga la kimaumbile la zilzala na kuongeza kuwa, "ujio wako wakati huu ambapo kuna hali hasasi katika eneo, una maana ya ndani ya kisiasa."