Askari wa Kizayuni wavamia al-Aqsa na kuwafukuza Waislamu
Waumini wa Kiislamu wametimuliwa katika Msikiti wa al-Aqsa baada ya Wazayuni wenye misimamo mikali wakiwa wameandamana na askari wa utawala haramu wa Israel kulivamia eneo hilo tukufu la Waislamu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la WAFA, walowezi hao wa Kizayuni walivamia msikiti huo jana Jumapili, wakati waumini hao wa Kiislamu walipokuwa wakitekeleza ibada zao katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetoa taarifa ya kulaani uvamizi huo, na kuutaka utawala wa Kizayuni ukomeshe tabia yake ya kuvamia na kuvunjia heshima maeneo matukufu ya Wapalestina katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.
Juzi pia, askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel walivamia Msikiti wa al-Aqsa na kuwatia nguvuni Wapalestina kadhaa waliokuwa kwenye Itikafu na ibada zingine za mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Msikiti wa al-Aqsa, ikiwa ndio nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina katika mji wa Baitul Muqaddas daima umekuwa ukiandamwa na hujuma na vitendo vya uharibifu vya utawala ghasibu wa Kizayuni.
Madhumuni ya hujuma na uvamizi huo unaoendelea kila uchao ni kuandaa mazingira ya kutekeleza mpango mwovu wa kuugawanya msikiti mtukufu wa al-Aqsa kimahali na kiwakati katika matumizi baina ya Waislamu na Mayahudi, ili hatimaye Wazayuni waweze kuudhibiti kikamilifu msikiti huo na kuchukua hatua zinazolenga kuuyahudisha na kuubomoa na kujenga kwenye magofu yake hekalu la uzushi la Kiyahudi.