Serikali ya Tunisia yaongeza muda wa hali ya hatari
Muda wa hali ya hatari nchini Tunisia unamalizika leo Jumanne. Jana Jumatatu Rais wa Tunisia alitangaza kuongeza muda wa hali hiyo ya hatari kwa mwezi mmoja zaidi.
Rais Beji Caid Essebsi jana alitoa taarifa na kusema kuwa, kuanzia leo Jumanne, hali ya hatari nchini Tunisia itaongezewa muda hadi mwezi mmoja mwingine.
Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, serikali ya Rais Beji Caid Essebsi iliongeza muda wa hali ya hatari kwa miezi mitatu zaidi.
Serikali ya Tunisia ilitangaza hali ya hatari baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi tarehe 24 Novemba mwaka jana dhidi ya basi lililokuwa na askari wa ulinzi wa Rais katika mji mkuu wa nchi hiyo Tunis.
Katika miezi ya hivi karibuni pia, nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imeshuhudia wimbi kubwa la mashambulio ya mabomu na ya kigaidi. Wiki kadhaa zilizopita pia, magaidi walifanya shambulio katika mji wa Bin Qirdan (Ben Gardane) na kuua watu 45.
Ikumbukwe kuwa idadi kubwa ya wanachama wa genge la kigaidi la Daesh ni raia wa Tunisia. Hivi sasa genge hilo linatumia fura ya kutokuweko serikali yenye nguvu katika nchi jirani ya Libya kutoa mafunzo ya kigaidi kwa wanachama wake ambao hufanya mashambulizi katika nchi mbalimbali kama vile Tunisia. La kufahamu ni kuwa, Libya na Tunisia zina mpaka wa takriban kilomita 500.