Vijana wa Kizayuni wakataa kuhudumu jeshini Israel
Vijana wa Kizayuni wameripotiwa kuzichoma moto barua wanazotumiwa kwa ajili ya kufanya kazi katika jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sambamba na hayo maandamano ya kupinga sera za Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni yanaendelea kwa muda sasa na yamepanuka hadi katika taasisi za kijeshi na kiusalama za utawala huo ghasibu. Wakati huo huo idadi kubwa ya maafisa na wanajeshi wametangaza kwamba hawako tayari tena kulituikia jeshi la utawala huo.
Licha ya kufungwa jela, vijana wa utawala wa Kizayuni wamezitia moto barua zao za kwenda kutumikia jeshi la Israel na wamekataa katakata kujiunga na jeshi hilo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema kuwa, kitendo cha vijana hao kukataa kwenda kulitumikia jeshi kina maana ya mwisho wa utawala huo.
Itafahamika kuwa, wanawake wa Israel wanapasa kuhudumu jeshini kwa muda wa miaka miwili na wanaume miaka mitatu. Huko nyuma pia mamia ya maafisa na askari wa kitengo cha "Cyber Espionage", kikosi chenye askari 8,200, walitangaza kujiuzulu kazi kwenye kikosi hicho wakipinga hatua ya baraza la mawaziri la Netanyahu ya kutekeleza mpango wa marekebisho ya sheria za mahakama ndani ya utawala huo ghasibu.