Jibu la kishujaa la binti wa Kipalestina kwa jinai za Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i97018-jibu_la_kishujaa_la_binti_wa_kipalestina_kwa_jinai_za_wazayuni
Binti mmoja wa Palestina ametekeleza operesheni ya kishujaa ya kujitoa kufa shahidi ili kujibu jinai za mtawalia za wanajeshi makatili wa Israel na walowezi wa utawala huo pandikizi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 05, 2023 05:02 UTC
  • Jibu la kishujaa la binti wa Kipalestina kwa jinai za Wazayuni

Binti mmoja wa Palestina ametekeleza operesheni ya kishujaa ya kujitoa kufa shahidi ili kujibu jinai za mtawalia za wanajeshi makatili wa Israel na walowezi wa utawala huo pandikizi.

Mapema jana Alkhamisi asubuhi, tarehe 4 Mei, 2023, jeshi la utawala wa Kizayuni lilitangaza kuwa limewaua shahidi wanamapambano wawili wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS wanaojulikana kwa majina ya Hassan Qatani na Muadh al Masri wakiwa pamoja na Ibrahim Jabri, Mpalestina mwingine aliyewasaidia wanaharakati hao wawili wa HAMAS kupata sehemu ya kujificha. Wanamapambano hao wa Palestina walifanya operesheni ya kishujaa ya Al-Āghwār na kuangamiza walowezi watatu wa Kizayuni takriban mwezi mmoja uliopita. Majibu kutoka kwa wanamapambano wa Palestina dhidi ya Wazayuni yametolewa katika kipindi kifupi mno mara baada ya jeshi la Israel kufanya jinai ya kuwaua shahidi wanaharakati hao watatu wa Palestina, kinyume na ulivyotarajia utawala wa Kizayuni. Vyombo vya habari vya Kizayuni vimetangaza kuwa, binti mmoja Mpalestina mwenye umri wa miaka 26 amelipiza kisasi cha jinai hiyo ya Wazayuni ingawa na yeye mwenyewe amejeruhiwa kwa risasi na muda mfupi baadaye amekufa shahidi.

Operesheni hiyo ya kishujaa ya binti huyo wa Kipalestina ina nukta kadhaa za kutiliwa maanani.

Baada ya kumpiga risasi wanajeshi wamezuia binti huyo aliyejeruhiwa wa Kipalesina kupewa huduma ya kwanza

 

Kwanza operesheni hiyo imethibitisha kuwa jinai yoyote ya Wazayuni haiwezi kuachwa vivi hivi bila ya kujibiwa na taifa shujaa la Palestina. Jengine ni kuwa majibu kwa jinai hizo za Wazayuni hayawahusu wanaume tu bali hata wanawake Wapalestina ni jinamizi kwa utawala mtenda jinai wa Kizayuni.

Vile vile operesheni hiyo ya binti wa Kipalestina imethibitisha kuwa, Wapalestina wote wanakubaliana kwa kauli moja juu ya wajibu wa kujibiwa jinai zote za Wazayuni. Msimamo huo ni jinamizi jingine kwa serikali yenye misimamo mikali kupindukia inayoongozwa na Benjamin Netanyahu huko Tel Aviv.

Suala jingine ni kwamba, operesheni hiyo ya binti wa Palestina inaonesha kuwa, Wapalestina wanao uwezo wa kujibu jinai za Wazayuni haraka sana, kadiri inavyowezekana. Wazayuni walifanya jinai ya kuwaua shahidi wanaharakati hao watatu wa Palestina jana asubuhi huko Nablos, jioni ya jana hiyo hiyo, binti huyo wa Kipalestina ameendesha operesheni ya kujibu jinai hiyo ya Wazayuni. Majibu hayo ya haraka sana ni uthibitisho kuwa Wapalestina wako tayari kwa lolote na muda wote. Ni uthibitisho pia kwamba, mapambano ya ukombozi wa Palesitna pamoja na makundi ya muqawama kama Hamas, Jihad al Islami na mengineyo, yanaungwa mkono vilivyo na wananchi wa Palestina.

Jinai za Wazayuni zinanyamaziwa kimya na madola ya Magharibi yanayojifanya kutetea haki za binadamu

 

Operesheni ya kishujaa ya jana jioni ya binti huyo wa Palestina imefanyika katika hali ambayo, hivi sasa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel zinatawaliwa na serikali yenye misimamo mikali kupindukia ya Kizayuni. Serikali hiyo ya nduli na watenda jinai Wazayuni, haisiti kufanya jinai yoyote ile dhidi ya Wapalestina. Lakini misimamo hiyo mikali na ukatili huo wa kupindukia wa Wazayuni haujawazuia vijana wa Palestina kuendeleza muqawama na mapambano yao dhidi ya Wazayuni maghasibu. Msimamo huo unatembea katika mishipa ya damu ya kila Mpalestina.

Nukta ya kumalizia hapa ni kwamba, wanajeshi makatili wa Israel walimjeruhi binti huyo Mpalestina jana jioni na wakamzunguka wote wakiwa na silaha kali naye ameanguka chini na kuzuia asifikishiwe msaada wa aina yoyote ile. Wapalestina wameandika kuwa, wanajeshi makatili wa Israel walizuia kwa makusudi kusaidiwa binti huyo hadi alipokufa shahidi. Kitendo hicho chenyewe cha Wazayuni ni jinai kubwa inayokanyaga sheria zote za kimataifa na haina chembe ya ubinadamu. Lakini pamoja na wanajeshi wa Israel kufanya jinai yote hiyo, madola ya kibeberu ya Magharibi yanayodai ni viranja wa kutetea haki za binadamu, si tu yanaendelea kunyamazia kimya jinai hizo, bali hata yanaziunga mkono waziwazi kwa maneno ya kibazazi, na kila Umoja wa Mataifa unapoamua kupasisha azimio dogo tu la kulaani jinai za Wazayuni, madola hayo ya kiistikbari hasa Marekani yanatumia kura ya veto kufelisha azimio hilo.