WHO yatakiwa kusaidia kuachiliwa huru mateka wa Kipalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i97622-who_yatakiwa_kusaidia_kuachiliwa_huru_mateka_wa_kipalestina
Kamati ya Wafungwa wa Kipalestina imelitaka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuingilia kati na kuokoa roho za mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya kuogofya ya utawala vamizi wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 21, 2023 10:09 UTC
  • WHO yatakiwa kusaidia kuachiliwa huru mateka wa Kipalestina

Kamati ya Wafungwa wa Kipalestina imelitaka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuingilia kati na kuokoa roho za mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya kuogofya ya utawala vamizi wa Israel.

Kamati hiyo imelitaka Shirika la Afya Duniani (WHO) kutuma timu ya wataalamu katika magereza ambayo Wapalestina wanashikiliwa mateka ili kuchunguza hali zao za kiafya hasa kutokana na kuweko ripoti kwamba, afya za wengi wao haziridhishi.

Mwito huo unatolewa katika hali ambayo, ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, kuna mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya utawala haramu wa Israel ambao licha ya kuugua maradhi mbalimbali, lakini maafisa magereza wamekuwa wakizuia Wapalestina hao kupatiwa matibabu.

Katika miezi ya hivi karibuni, utawala haramu wa Israel kupitia maafisa wake wa magereza, umeshadidisha ukandamizaji wake dhidi ya wafungwa wa Kipalestina, unyama ambao umekabiliwa na malalamiko makubwa ya walimwengu kieneo na kimataifa.

Zaidi ya wafungwa 7,000 wa Kipalestina kwa sasa wanazuiliwa katika takriban jela 17 za utawala haramu wa Israel. Mamia ya wafungwa, wakiwemo wanawake na watoto wadogo, wanazuiliwa bila kufunguliwa mashtaka hatua ambayo imeendelea kulaaniwa vikali na makundi ya kutetea haki za binadamu.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, utawala haramu wa Israel umewatia mbaroni zaidi ya wanawake 16,000 wa Kipalestina tangu mwaka 1967 huku mashirika ya haki za binadamu yakionya kuhusu hali mbaya ya wafungwa wa kike katika jela za kuogofya za Israel.