Wayemen wafanya maandamano makubwa katika Siku ya Kupambana na Uistikbari
Wananchi wa Yemen leo Jumatano wamekusanyika katika maidani kuu ya mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a na katika miji mingine ya nchi hiyo kufanya maandamano makubwa kwa mnasaba wa Siku ya Kupambanan na Uistikbari yaani "Yaum Sarkha."
Tarehe ya kuadhimisha Siku ya Kupambana na Uistikbari huko Yemen inarejea hadi tarehe 17 Januari 2002; na katika uwanja wa madrasa ya kielimu ya Imam Hadi A.S huko Sana'a; ambapo katika siku hiyo Sayyid Hussein al Houthi Kiongozi shahidi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen alitoa hutoba yake maarufu chini ya anwani "Mayowe dhidi ya Waistikbari". Katika hotuba hiyo, Sayyid Hussein al Houthi alisema: Sisi kama Waislamu hatuziruhusu Marekani na Israel kumtawala hata Muislamu mmoja.
Wananchi wa Yemen mwaka huu pia wamefanya maandamano huku wakipiga nara dhidi ya mababeru wa dunia na kupeperusha bendera ya Yemen. Wananchi hao wamesisitiza juu ya ulazima wa kususiwa bidhaa za Marekani.
Katika maandamano hayo ya leo, wananchi wa Yemen walikuwa wamebeba vitambaa na mabango yenye maandishi yanayosema "tunaalani sera za kivamizi za Marekani na utawala wa Kizayuni", na kusisitiza uungaji mkono wao kwa wananchi na kadhia ya Palestina mkabala wa hujuma za maghasibi Wazayuni.
Maandamano hayo yamefanyika katika mikoa mingine na miji mikubwa ya Yemen ikiwemo Saada, Hajjah, Dhamar, Taiz, Imran, Ab, Rime, Al Jawf, al Mahwit, Al-Dhale, al Bayda na Maarib. Wakazi wa mkoa wa al Hudaydah pia leo alasiri walifanya maandamano sawa na hayo yaliyoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali huko Yemen.