UN: Watoto nusu milioni wa Yemen wanakabiliwa na utapiamlo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i98108-un_watoto_nusu_milioni_wa_yemen_wanakabiliwa_na_utapiamlo
Mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yameonya kuwa, watoto zaidi ya laki tano wa Yemen wanawajihiwa na utapiamlo wa kiwango cha juu, hali inayotishia maisha yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 28, 2023 03:14 UTC
  • UN: Watoto nusu milioni wa Yemen wanakabiliwa na utapiamlo

Mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yameonya kuwa, watoto zaidi ya laki tano wa Yemen wanawajihiwa na utapiamlo wa kiwango cha juu, hali inayotishia maisha yao.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya pamoja ya Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Shirika la Chakula na Kilimo la umoja huo FAO na Shirika la Chakula Duniani WFP.

Ripoti ya mashirika hayo ya UN imebainisha kuwa, watoto zaidi ya nusu milioni watakabiliwa na utapiamlo mkali mwaka huu 2023 katika majimbo ya kusini mwa Yemen, ambapo laki moja miongoni mwao wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na kiwango cha kutisha cha utapiamlo.

Kadhalika ripoti hiyo imeeleza kuwa, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wapatao 250,000 wanaandamwa pia na utapiamlo mkali katika maeneo hayo ya Yemen.

Kwa mujibu wa takwimu za UNICEF, watoto milioni 11 wanahitaji misaada ya kibinadamu huko Yemen na kwamba kati ya idadi hiyo, watoto zaidi ya laki tano na arubaini elfu walio na umri wa chini ya miaka mitano wanasumbuliwa na utapiamlo mkali.

Kituo cha Haki za Binadamu cha Ain kiliwahi kuripoti kuwa, raia wa Yemen 18,140 wameuawa na wengine elfu 30,254 wamejeruhiwa katika kipindi cha miaka minane ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo maskini ya Kiarabu.