Wairaqi walaani njama za Marekani za kutaka kuwaua viongozi wa muqawama
Wananchi wa Iraq wamefanya maandamano katika mji mkuu Baghdad, kupinga na kulaani uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, na vile vile njama za Washington za kutaka kuwaua kigaidi viongozi wa kambi ya muqawama nchini humo.
Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kutaka kukomeshwa chokochoko hizo za Marekani nchini kwao, wamemkosoa vikali Alina Romanowski, Balozi wa Marekani mjini Baghdad kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Waandamanaji hao waliokusanyika karibu na ubalozi wa Marekani katika eneo lenye ulinzi mkali la 'Green Zone' mjini Baghdad, wameitaka serikali ya nchi yao na hasa Bunge litoe tamko hadharani kuhusu misimamo yao kwa ubalozi wa Marekani nchini humo.
Wananchi wa Iraq walioshiriki katika maandamano hayo ya jana Ijumaa wametoa mwito wa kufanyika maandamano makubwa zaidi kulaani uingiliaji huo wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, na vile vile njama za Washington za kutaka kuwaua kigaidi viongozi wa mrengo wa muqawama katika eneo.
Vyombo vya habari vya Marekani viliripoti hivi karibuni kuwa, Washington inapanga kuwaua wakuu wa makundi ya muqawama nchini Iraq, hasa viongozi wa Harakat Hizbullah al-Nujaba.
Maafisa wa Washington wanadai kuwa, harakati hiyo ya mapambano ilihusika na shambulio la ndege zisizo na rubani (droni) lililolenga wanajeshi wa Marekani nchini Syria mwezi Machi mwaka huu.
Wananchi wa Iraq wamekuwa wakikosoa uingiliaji wa madola ya Magharibi hususan Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo pamoja na nchi nyingine za Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, uingiliaji huo kamwe hauwezi kuwa suluhu ya matatizo na changamoto za eneo hili.