Korea Kaskazini yavurumisha makombora kujibu uchokozi wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i100086-korea_kaskazini_yavurumisha_makombora_kujibu_uchokozi_wa_marekani
Korea Kaskazini imevurumisha makombora mawili ya balestiki kuelekea Bahari ya Mashariki kujibu chokochoko za Marekani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 19, 2023 10:09 UTC
  • Korea Kaskazini yavurumisha makombora kujibu uchokozi wa Marekani

Korea Kaskazini imevurumisha makombora mawili ya balestiki kuelekea Bahari ya Mashariki kujibu chokochoko za Marekani.

Shirika la habari la Yonhap limeripoti kuwa, Pyongyang mapema leo Jumatano imefyatua makombora mawili ya balestiki yaliyodondoka katika Bahari ya Mashariki (Bahari ya Japan), kama jibu kwa hatua ya kichokozi ya Washington ya kutuma nyambizi iliyosimikwa silaha za nyuklia katika bandari ya Korea Kusini.

Mkuu wa Majeshi ya Korea Kusini amethibitisha habari za kuvurumishwa makombora hayo na kueleza kuwa, yamefyatuliwa kutoka eneo la Sunan viungani mwa Pyongyang, pwani ya mashariki ya nchi hiyo na kudondoka katika Bahari ya Japan.

Japan pia imethibitisha habari hizo za kuvurumishwa makombora ya balestiki na Korea Kaskazini, hatua ambayo Pyongyang inasema ni muendelezo wa majaribio ya silaha zake kujibu hatua ya US ya kutuma silaha za nyuklia Korea Kusini, na luteka za kijeshi za mara kwa mara zinazofanywa na Washington na Seoul.

Korea Kaskazini imekuwa ikiendelea kustawisha uwezo wake wa silaha za makombora tangu yalipokwama mazungumzo ya kuishinikiza itokomeze silaha zake za nyuklia na makombora ya balestiki, mkabala wa kupunguziwa vikwazo vilivyolemaza uchumi wa nchi hiyo.

Korea Kaskazini imesema itatoa jibu mwafaka kwa makubaliano ya hivi karibuni baina ya Washington na Seoul, ya kuiruhusu Marekani kutuma manowari zilizoshehenezwa kwa silaha za nyuklia katika Peninsula ya Korea.